Jun 04, 2022 09:05 UTC
  • Fikra za Imam Khomeini (MA); ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuanza mwamko wa Kiislamu

Fikra za Imam Khomeini MA za kupambana na ubeberu, mbali na kupelekea kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, zimepelekea pia kupatikana mwamko wa Kiislamu katika eneo hili zima na duniani kwa ujumla.

Miaka 33 iliyopita, Sayyid Ruhullah Mousavi Khomeini MA, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran alifariki dunia baada ya kupitisha miaka 87 ya umri uliojaa juhudi zisizochoka.

Mwaka 1963, Imam Khomeini MA alianzisha harakati zake dhidi ya utawala wa kidikteta wa mfalme Shah na ubeberu wa Marekani nchini Iran. Utawala wa Shah ambao ulishindwa kuvumilia harakati za ukombozi za Imam Khomeini MA, ulimbaidisha mwanachuoni huyo mwanamapambano na kumlazimisha kwenda kuishi Uturuki na baadaye nchini Iraq.

Imam Khomeini alipitisha miaka 13 ya kuwa ubaidishoni nchini Iraq, lakini aliendeleza harakati zake na kuandaa mazingira ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini. Hatimaye mwaka 1979, wananchi wa Iran kwa uongozi wa hekima na busara kubwa wa Imam Khomeini MA, walifanikiwa kuuangusha utawala wa kiimla wa Shah ambao ulikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo hili. Ushindi huo ulileta matumaini makubwa kwa mataifa ya wanyonge duniani na hapo hasa ndipo ulipoanza mwamko wa kweli wa Kiislamu wa kupambana na uistikbari wa madola ya kibeberu.

Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Tunapozitupia jicho fikra za Imam Khomeini MA tutaona kuwa, msingi mkubwa wa fikra hizo ni kwamba Uislamu unao uwezo wa kuleta mabadiliko na mapinduzi ya pande zote kwa mtu binafsi na kwa jamii tena katika nyuga zote za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kisayansi, kiteknolojia n.k. Ni kwa fikra na misingi hiyo ndio maana Imam Khomeini alifanikiwa kuongoza mapinduzi makubwa zaidi ya karne hii na kukata mikono ya wezi wa Magharibi na Mashariki mwa dunia ambao walikuwa wanapora utajiri wa vitu na wa kiroho wa taifa la Iran. 

Msingi mkuu wa fikra ya Imam Khomeini MA ni mafundisho ya dini tukufu ya KIislamu na fikra hiyo ilibadilika kuwa ratiba ya kivitendo ya kusukuma mbele mambo ya muhimu sana. Fikra hiyo ni ya kupiga vita ubeberu wa Magharibi, kupambana na ukoloni, kuleta umoja na mshikamano katika safu za Waislamu na kuunda utawala wa kimataifa.

Wakati mfumo wa kiistikbari duniani ulipokuwa tayari umeshayatwisha mataifa ya dunia fikra zake za kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi, Imam Khomeini MA alidhihiri na kufanikisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akaleta mikakati mipya inayotekelezeka kivitendo iliyosimama juu ya mafundisho sahihi ya Uislamu, kumwangalia mwanadamu kimataifa na kuja na mkakati wa kupiga vita ubeberu. Jambo hilo kwa hakika liliutumbukiza kwenye wakati mgumu sana uistikbari wa kimataifa, duniani. 

Mazingira yoyoite ya hali ya hewa hayawazuii wananchi wa Iran kujitokeza kwa mamilioni kila mwaka, kuamdhimisha siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini 

Kutokea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa wimbi kubwa ambalo jina lake ni mwamko wa Kiislamu na ambalo linaendea hadi hivi sasa, kutoka Asia Magharibi hadi barani Afrika, bara ambalo wananchi wake wengi wana uzoefu mchungu kwa kutawaliwa kikoloni na kibeberu na madola ya Magharibi. Mwamko huo wa Kiislamu umepelekea pia kusambaratishwa tawala za kiimla za nchi kadhaa za Afrika kama Tunisia na Misri pamoja na kuziweka kwenye wakati mgumu tawala za vibaraka wengine kama Bahrain. 

Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana wasomi na wanafikra wengi wa nchi za Magharibi wakasema kuwa, Imam Khomeini alifufua matukufu ya Kiislamu na wanaamini kuwa, mwanachuoni huyo mwanamapambano alitekeleza kivitendo yale ambayo wapigania mabadiliko na marekebisho katika jamii za Kiislamu na mwandamu, walikuwa wakiona ni ndoto kuweza kutekelezwa fikra hizo kivitendo. Wasomi hao wa Magharibi ni pamoja na Profesa William Orman Beeman wa Marekani.

Naam, tunapoangalia kwa kina fikra za Imam Khomeini tunaweza kusema kuwa, uongozi wa mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ulioyafikisha kwenye ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupelekea kuanza wimbi la mwamko wa Kiislamu kwa kutegemea nguvu za wananchi ukiwa ndio msingi mkubwa wa mapinduzi mbalimbali yenye harufu na rangi ya kimaanawi, aidha kutokana na fikra hizo kumtanguliza mbele  Mwenyezi Mungu katika kila kitu, na kaulimbiu yake kuu ya "Si Mashariki, Si Magharibi; Bali ni Jamhuri ya Kiislamu" yote hayo ni nakala ya kumpa ushindi mwanadamu na ni chombo bora cha kuweza kupambana na maadui wa Uislamu, kuwakomboa watu wanaodhulumiwa duniani na pia kukabiliana vilivyo na ubeberu wa madola ya kiistikbari.

Tags