Jun 05, 2022 09:52 UTC
  • Kamanda: Maadui wamekiri kusambaratika njama zao dhidi ya Iran

Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kuwa, "maadui wamekiri kuwa njama zao dhidi ya Iran zimefeli na kusambaratika."

Admeri Ali Fadavi, Kaimu Kamanda Mkuu wa IRGC ameyasema hayo leo alipohutubu katika hadhara ya kumbukumbu ya Mwamko wa 15 Khordad iliyofanyika katika Haram Takatifu ya Imamzadeh Ja'afar bin Musa al Kadhim katika eneo la Pishva eneo la kusini mashariki mwa Tehran.

Ikumbukwe kuwa, Juni 5 1963 (Khordad 15 13 42 Hijria Shamsia) wananchi wa Iran waliandamana katika miji mbali mbali kulalamikia hatua ya utawala wa kiimla wa Shah ya kumkamata Imam Khomeini (MA). Maandamano katika miji ya Qum, Tehran na Varamin yalimalizika kwa umwagaji mkubwa wa damu kutokana na ukatili wa vikosi vya kijeshi ambavyo viliwaua shahidi watu kadhaa. Sikuu hii ni maarufu kama Mwamako wa 15 Khordad.

Akizungumza kwa mnasaba wa kukumbuka mwamko huo, Admeri Fadavi amesema: "Miaka 42 baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, makhabithi wa dunia kinara wao akiwa ni Marekani si tu kuwa hawajafanikiwa katika njama zao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali pia wanakiri kushindwa katika njama zao hizo."

Maandamano ya wananchi wa Iran katika mwamko wa 15 Khordad

Kamanda huyo mwandamizi wa IRGC amesema mrengo wa kufri umechukua kila aina ya hatua dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini pamoja na hayo haujaweza kufanikiwa.

Admeri Fadavi ameendelea kusema kuwa, pamoja na kuwepo njama zote za Marekani na waitifaki wake lakini Iran imeweza kusimama kidete mbele ya hujuma na mrengo huo wa kufri na dhulma.

Kaimu Kamanda Mkuu wa IRGC amesema Marekani na waitifaki wake hawajawahi kuacha hata sekunde moja njama zao khabithi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini pamoja na hayo leo Jamhuri ya Kiislamu ni imara na yenye nguvu zaidi.

 

Tags