Jun 11, 2022 07:27 UTC
  • Balozi Zubairu Dada katika mazungumzo yake na Rais Ebrahim Raisi mjini Tehran
    Balozi Zubairu Dada katika mazungumzo yake na Rais Ebrahim Raisi mjini Tehran

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria amesema kuwa, nchi za Kiislamu na Waislamu wote kwa ujumla wanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja katika vita vya kuangamiza fikra potofu ya ukufurishaji.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kumnukuu Zubairu Dada, Waziri wa Nchi wa Shirikisho la Nigeria katika Masuala ya Kigeni akisema hayo hapa mjini Tehran ambapo amekuja kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha sita cha pamoja na kamati ya pamoja ya Iran na Nigeria.

Alisema hayo jana Ijumaa wakati alipoonana na Mkuu wa Mkoa wa Qum wa kusini mwa Tehran, Sayyid Mohamad Taqi Shahcheragh na huku akigusia jinai zinazofanyewa na magenge ya ukufurishaji kama Boko Haram huko Nigeria amesema, haiwezekani kupambana na fikra ya ukufurishaji na majoka hayo yanayoogofya bila ya kuweko mshikamano wa kweli kati ya Waislamu wote.

Bendera za Iran na Nigeria

 

Waziri huyo wa nchi wa Nigeria katika masuala ya kigeni vile vile ameelezea kufurashishwa kwake na ziara yake hapa nchini Iran na kusisitiza kwa kusema: Kwa vile mimi ni Muislamu, ni wajibu wangu kujua mengi kuhusu dini yangu na madhehebu zake likiwemo la Kishia.

Zubairu Dada amezungumzia idadi kubwa ya Waislamu wa Kishia walioko nchini Nigeria na kusema kuwa, kuna suutafahamu ilijitokeza kuhusu Waislamu wa Kishia nchini Nigeria wakati ambapo Katiba ya Nigeria inaheshimu itikadi zote,hata za wale watu ambao hawaamini kabisa kuweko Mwenyezi Mungu lakini wanaishi kwa utulivu na Wanigeria wengine bila ya kusababisha matatizo yoyote.

Amesema, amefurahishwa na kuona watu wa itikadi zote wanaishi kwa utulivu na amani kikamilifu nchini Iran na kusema ana matumaini uhusiano wa Nigeria na Iran utazidi kuimarika katika nyuga zote.

Tags