Jun 12, 2022 04:44 UTC
  • Abdollahian: Iran haina vizingiti katika kukuza ushirikiano wake na Nigeria

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haina vizingiti vyovyote katika njia ya kustawisha uhusiano wake na Nigeria.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Zubairu Dada, Waziri wa Nchi wa Shirikisho la Nigeria katika Masuala ya Kigeni na kusisitiza kwamba, taifa hili halina mipaka katika kukuza na kustawisha uhusiano wake na Abuja.

Abdollahian amesisitiza kuwa, Iran inakaribisha kwa mikono miwili juhudi za kuimarishwa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi za Kiislamu katika nyaja zote hususan katika uga wa kiuchumi na kibiashara.

Aidha amesema, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya pande mbili hakiendani kabisa na suhula zilizopo katika nchi hizi mbili na kiko bali na kiwango kinachotakiwa.

Zubairu Dada, Waziri wa Nchi wa Shirikisho la Nigeria katika Masuala ya Kigeni katika mazungumzo yake na Rais Ibrahin Raisi

 

Kadhalika Hussein Amir-Abdollahian amekumbushia azma ya serikali ya sasa ya awamu ya 13 ya kuimarisha ushirikiano na mataifa ya Kiafrika na hasa Nigeria.

Kwa upande wake, Zubairu Dada, Waziri wa Nchi wa Shirikisho la Nigeria katika Masuala ya Kigeni ameonyesha kuridhishwa mno na safari yake hapa Iran na kubainisha kwamba, nchi yake iko tayari kuongeza ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ambavyo ameeleza kwamba, tuna matarajio katika mustakabali usio mbali tutashuhudia kupanuliwa ushirikiano zaidi baina ya mataifa haya mawili katika nyaja mbalimbali. 

Tags