Jun 12, 2022 09:03 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu kuwa mapambano ndio njia pekee ya kufikia ushindi dhidi ya Marekani

Akizungumza jana Jumamosi alasiri katika kikao na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na ujumbe alioandamana nao, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya kusimama imara Iran na Venezuela mbele ya mashinikizo makali na vita vya pande kadhaa vya Marekani na kusisitiza: Uzoefu wa mafanikio wa nchi mbili unaonyesha kwamba njia pekee ya kukabiliana na mashinikizo hayo ni mapambano na kusimamam imara.

Ayatullah Khamenei ameashiria maendeleo na ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni, na kuongeza kuwa: "Hatua hizo kubwa zimefikiwa katika hali ambayo taifa la Iran limekuwa chini ya vikwazo na mashinikizo makubwa zaidi yasiyo na mfano wake, ambayo yametajwa na Waamerika wenyewe kuwa  "mashinikizo ya juu kabisa." Pamoja na hayo lakini mapambano ya watu wa Iran yamepelekea kushindwa mashinikizo hayo ya juu, kadiri kwamba mmoja wa maafisa mashuhuri wa kisiasa wa Merikani hivi karibuni alikutaja kushindwa huko kuwa ni "kushindwa kwa fedheha".

Iran na Venezuela katika miongo ya hivi karibuni zimekuwa zikiwekewa vikwazo mbalimbali vya upande mmoja vya Marekani kutokana na sera zao za kupinga ubabe na ubeberu wa nchi hiyo ya Magharibi. Hususan, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imekuwa chini ya vikwazo vya Marekani tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kutekwa nchini pango la ujasusi la Marekani mwaka 1979 katika kipindi cha utawala wa Rais Jimmy Carter wa nchi hiyo. Vikwazo hivyo vimeimarishwa tangu mwaka 2000 kwa kisingizio cha kukabiliana na mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

Mafisa wa Iran na Venezuela kwenye mazungumzo hayo

Isitoshe vikwazo hivyo viliongezwa na kufikia kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha utawala wa Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, aliyeiondoa nchi hiyo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuweka vikwazo vikali na visivyo na mfano wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hoja ya kuifanya Iran isalimu amri mbele ya matakwa haramu na yasiyo ya kimantiki ya Washington kuhusiana na suala zima la nyuklia, uwezo wa makombora ya Iran na siasa zake za kieneo.

Hata hivyo, kampeni hiyo ya kidhalimu imeshindwa vibaya, suala ambalo hata wanasiasa na maafisa wakuu wa Marekani wamelikiri hadharani. Seneta Chris Murphy wa chama cha Democrat amekiri kwamba mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran yamekuwa bila natija na wala hayajazaa matunda yoyote ya maana. Seneta huyo wa Marekani amekiri wazi kushinindwa vikwazo na mashinikizo hayo ya Marekani na kusisitiza kuwa hayajakuwa na matunda yoyote kwa Washington. Amesema: Marekani haijanufaika kwa njia yoyote ile na vikwazo na mashinikizo ya juu yaliyowekwa na serikali ya Trump. Kukiri kwa Seneta huyo wa Marekani kuhusu kushindwa kampeni ya kuiwekea Iran vikwazo na mashinikizo ya juu kumetimia sambamba na kukiri jambo hilo maafisa wakuu wa utawala wa sasa wa Marekani.

Katikati ya mwezi Januari mwaka huu, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani Jake Sullivan alikiri kwamba Washington ilikuwa inalipa gharama ya makosa makubwa yaliyofanywa na Trump kuhusu mapatano ya JCPOA. Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kama alivyofanya Sullivan, pia amekiri makosa ya kimkakati yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na utawala wa Marekani kuhusu kujiondoa katika mapatano hayo. Mnamo Desemba 7 mwaka uliopita, Blinken alisema kujiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia ya 2015 lilikuwa ni kosa kubwa. Hata Robert Malley, mshiriki mkuu wa Marekani katika mazungumzo ya Vienna juu ya kuiondolea Iran vikwazo, amekiri juu ya kushindwa mashinikizo ya juu ya Washington dhidi ya Tehran.

Ras Maduro (kushoto) akiwa na mwenyeji wake Rais Ebrahim Raisi wa Iran mjini Tehran

Kuhusu Venezuela pia, Marekani iliendeleza sera ya kushinikiza kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayati Hugo Chavez tangu kuapishwa kwake kwa kuiwekea serikali yake vikwazo mbali mbali. Mwenendo huo uliendelezwa na ungali unaendelezwa katika kipindi cha uongozi wa rais wa hivi sasa wa nchi hiyo Nicolas Maduro. Hata hivyo, Venezuela imesimama imara mbele ya mashinikizo na vikwazo hivyo vya kidhalimu vya Marekani kwa usaidizi na msaada wa nchi rafiki na hasa Iran. Kwa msaada huo Vinezuela imeweza kusimama mbele ya Washington ambayo inatumia wapinzani vibaraka wa ndani ya Venezuela, na hasa wale wanaoongizwa na Juan Guido kwa lengo la kutaka kuipindua serikali halali ya nchi hiyo na kujaribu kuitenga kieneo na kimataifa. Kuhusiana na hilo, Nicolas Maduro sambamba na kushukuru uungaji mkono wa Iran katika mapambano makali ya taifa la Venezuela dhidi ya Marekani amesema: “Mlitusaidia wakati hali ya Venezuela ilikuwa ngumu sana na hakuna nchi yoyote iliyokuwa tayari kutusaidia, lakini nyinyi mlitusaidia na kutuwezesha kutoka kwenye hali hiyo."

Hivi sasa, kufuatia ziara ya Rais wa Venezuela nchini Iran, milango mipya ya ushirikiano wa pande mbili kwa ajili ya kuboresha kiwango cha uhusiano na kuratibu njia za kukabiliana na hatua haribifu za Marekani imefunguliwa. Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei amekaribisha kutiwa saini hati ya ushirikiano wa miaka 20 kati ya Iran na Venezuela. Kiongozi Muadhamu  wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ushirikiano wa muda mrefu unahitajia kufuatiliwa na kutekelezwa kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa. Akizungumzia ushirikiano wa dhati  na kirafiki uliopo kati ya Iran na Venezuela amesema: "Hakuna nchi zilizo na uhusiano wa karibu kama nchi mbili hizi, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha kivitendo kwamba iko tayari kujihatarisha na kushika mikono ya marafiki zake inapohitajika kufanya hivyo."

Tags