Jun 15, 2022 07:31 UTC
  • Kwa mara nyingine, Iran yalaani jaribio la UK la kuwahamishia wakimbizi nchini Rwanda

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara nyingine tena amelaani jaribio la Uingereza la kuwahamishia kwa lazima wakimbizi wa nchi hiyo huko Rwanda na kusema kuwa hiyo ni aibu ya kihistoria.

Saeed Khatib Zadeh amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatano na kuongeza kuwa, jaribio la kuwapeleka wakimbizi hao katika nchi nyingine ni jambo la hatari na linaweza kusambaratisha sehemu iliyosalia ya mfumo wa kimataifa wa kuwalinda wakimbizi.

Huku hayo yakiripotiwa, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, serikali ya UIngereza imelazimika kuakhirisha dakika za mwisho safari ya kwanza ya ndege ya wakimbizi kutoka Uingereza kuelekea Rwanda baada ya Bunge la Haki za Binadamu la Ulaya kutoa amri ya kusimamishwa zoezi hilo. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatib Zadeh

 

Kabla ya hapo na baada ya serikali ya Uingereza kutangaza kuwa kundi la kwanza la wakimbizi waliokimbilia nchini humo lilipangiwa kupelekwa Rwanda jana Jumanne, jana hiyo hiyo serikali ya Kigali kupitia msemaji wake Bi Yolande Makolo ilisema kuwa, imejiandaa vizuri kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi hao.

Makubaliano hayo yamefikiwa baina ya serikali za Kigali na London baada ya Uingereza kushindwa kufikia makubaliano kama hayo na nchi za Kenya, Ghana na Albania. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza.

Kabla ya hapo pia, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Filippo Grandi, naye alikuwa amekosoa uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kuwahamishia Rwanda watafuta hifadhi wanaokimbilia nchini humo huku akisema makubaliano hayo ya kando kati ya nchi mbili hizo ni makosa.

Tags