Jun 16, 2022 09:28 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya kuimarishwa mahusiano ya Iran na Turkmenistan

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu alisema Jumatano ya jana wakati alipokutana na Rais Serdar Berdimuhamedow wa Turkmenistan na ujumbe aliofutana nao kwamba, kustawisha na kuimarishwa kadiri inavyowezekana uhusiano wa Iran na Turkmenistan ni kwa maslahi ya nchi mbili.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameeleza kuwa, kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa na majirani ni kipaumbele cha sera za kigeni za Iran, na sera hii ni nzuri na sahihi mno.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kusisitiza kwamba, sharti la kuvukwa vizingiti ni azma na irada thabiti ya nchi mbili kwa ajili ya kustawisha zaidi uhusiano ameongeza kwamba, bila shaka mahusiano ya kirafiki baina ya Iran na Turkmenistan yana upinzani katika uga wa kieneo na kimataifa, lakini kuna ulazima wa kuvuka vizuizi vilivyoko katika njia hii.

Kuna ulazima wa kuzifanya kuwa amilifu kamisheni za ushirikiano wa pamoja baina ya mataifa haya mawili na kisha kufuatilia bila kikomo makubaliano yaliyofikiwa na kisha kuhakikisha yanatekelezwa kivitendo.

Katika mazungumzo hayo ambapo Rais Ibrahim Raisi wa Iran alihudhuria pia, Rais Serdar Berdimuhamedow wa Turkmenistan alisema:  Serikali yake inatoa kipaumbele kuhusu suala la kuboresha uhusiano na mataifa jirani, na inafanya kila liwezekanalo kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu katika nyuga mbalimbali kama gesi, umeme, usafirishaji na uchukuzi, sanjari na kukamilisha miradi mikubwa, kwa misingi ya makubaliano yaliyosainiwa katika safari yake hii.

Iran imesaini mikataba tisa ya maelewano na Turkmenistan

 

Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, marais hao wawili walishiriki hafla ya kusainiwa mikataba tisa ya maelewano baina ya mataifa haya mawili katika nyuga mbalimbali kama uchumi na biashara, sayansi na teknolojia, utamaduni, mawasiliano, usalama na nishati.

Uhusiano wa Iran na Turkmenistan kwa kuzingatia utendajii wa sera za kigeni za serikali ya awamu ya 13 chini ya uongozii wa Rais Ebrahim Raisi ambayo inazingatia mno kuimarisha uhusiano na majirani, umo katika hali ya kukua, na safari ya Rais Serdar Berdimuhamedow wa Turkmenistan hapa Tehran na kukutana kwake na viongozi wa ngazi za juu hapa nchini inahesabiwa kuwa nukta muhimu katika uwanja huo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Turkmenistan zina uwezo mkubwa wa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali na kwa kuzingatia nafasi ya kijiografia ya Iran hilo ni kivutio kwa Turkmenistan kutokana na ufikiaji wake katika Bahari ya Caspian na Ghuba ya Uajemi, na hivyo kuwa fursa mwafaka kwa ajili ya usafirishaji na uchukuzi baina ya nchi mbili. Wakati huo huo mradi wa gesi wa Turkmenistan kwenda Jamhuri ya Azerbaijan kupitia Iran, ambao umekuwa ukifanya kazi tangu Januari mwaka huu (2022), ni dhamana na hakikisho la maslahi ya nchi mbili. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akizungumza na Rais wa Turkmenistan

 

Kwa mujibu wa mkataba huu, Iran kwa mwaka Iran inaikabidhi Azerbaijan mita za ujazo bilioni 1.5 hadi bilioni 2 za gesi ya Turkmenistan. Kuamilishwa diplomasia ya nishati na kustawishwa ushirikiano wa Iran na mataifa jirani katika uga wa nishati ni moja ya mipango iliyoko katika ajenda za Wizara ya Nishati ya Iran. Natija ya hilo ni kutiwa saini mkataba wa gesi tuliouashiria ambao licha ya kuwa kiwango chake ni kidogo, lakini kwa uoni wa weledi wa mambo hii ni hatua moja muhimu.

Hujjatullah Ghanimifard, mkurugenzi wa zamani wa masuala ya kimataifa katika Shirika la Mafuta la Iran anasema kuhusiana na mkataba huo kwamba: Kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi na kuongeza uzalishaji mafuta na gesi nchini, Iran inaweza kuthibitisha kuwa, siyo tu kwamba, ni muuzaji wa mafuta na gesi inayozalisha yenyewe, bali inaweza kuwa njia muhimu na salama kwa ajili ya kusafirishwa mafuta na gesi kuelekea mataifa jirani kwa njia mbalimbali.

Serikali ya awamu ya 13 inazipa kipaumbele nchi jirani katika sera zake za kigeni na Rais Ebrahim Rais tangu alipochukua hatamu za uongozi amekuwa akizingatia mno suala la ushirikiano mwema na majirani ikiwemo Turkmenistan. Kwa kuzingatia mipaka iliyopo baina ya Iran na Turkmenistan na kuweko fursa nyingi za kuinua kwango cha ushirikiano na mahusiano ya pande mbili, kama alivyoashiria pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwa, mahusiano ya nchi mbili yanapaswa kujengeka juu ya msingi wa maslahi ya pande mbili na kuchukuliwa hatua za kupanua na kustawisha zaidi uhusiano wao kadiri inavyowezekana.

Tags