Jun 23, 2022 02:23 UTC
  • Ukosoaji mkali wa Tehran dhidi ya ripoti ya UN kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran

Kamati ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa kujibu ripoti ya hali ya haki za binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye kikao cha 50 cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo.

Taarifa hiyo imeashiria jibu lenye kurasa zaidi ya 40 la Iran kwa rasimu ya ripoti ya UN na kusema: "Kumpa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kazi ya kutoa ripoti ya haki za binadamu kuhusu nchi makhsusi licha ya kuwepo taasisi husika za kimataifa na za kitaalamu si jambo la kimantiki na ni hatua isio ya kitaalamu.

Akitegemea madai yaliyotolewa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameibua masuala mbalimbali katika ripoti hiyo kiwa ni pamoja na kutoa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini. Guterres pia ameitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ishirikiane na ripota maalumu wa jumuiya hiyo kuhusu haki za binadamu.

Kamati ya Haki za Binadamu ya Iran imekosoa kitendo cha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa cha kuingiza siasa katika masuala ya haki za binadamu na kuhoji kwamba, kwa nini ripoti ya Antonio Guterres haikutaja au hata kuashiria Wairani wanaozuiliwa nje ya nchi?! Taarifa hiyo imekumbusha kuwa: Hatua ya Katibu Mkuu wa UN ya kuingiza siasa katika haki za binadamu inakiuka kanuni za wazi na za kimsingi za sheria na haki, ikiwa ni pamoja na "kanuni ya usawa wa watu wote mbele ya sheria" na "kanuni ya kutobagua."

Antonio Guterres

Taarifa hiyo ilikuwa ikiashiria Wairani wanaoshikiliwa na kuhukumiwa katika nchi kadhaa za Magharibi ikiwemo Sweden kwa tuhuma zisizo na msingi, suala ambalo halikutajwa walau kwa ishara tu katika ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa Tehran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba ripoti za haki za binadamu zinazotolewa dhidi ya Iran zinatokana na ushahidi wa kubuni na usio na mashiko yoyote.

Sambamba na hayo, nchi za Magharibi hasa Marekani ambayo ni miongoni mwa wavunjaji wakubwa wa haki za binadamu duniani, zimekuwa zikiunga mkono ripoti hizo zisizo za kweli. Kuhusiana na hilo, Robert Malley, mjumbe maalumu wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran, ametoa ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisifu utendaji wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, hususan ripota wa haki za binadamu nchini Iran.

Hii ni pamoja na kuwa, licha ya kaulimbiu za serikali ya Marekani kuhusu haki za binadamu na kutetea haki za mtu binafsi, za kijamii na vilevile uhuru na haki za kiraia, kesi nyingi za ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu nchini humo, kama vile mienendo isiyo ya kibinadamu, ukatili na ubaguzi wa wakazi asili, raia wenye asili ya Afrika na jamii za walio wachache, ikiwa ni pamoja na kutenganishwa watoto na wazazi wao, unyanyasaji usio na mipaka wala udhibiti wa polisi wa Marekani dhidi ya wasio wazungu, hali mbaya ya wafungwa na kadhalika, zinaonyesha uongo wa madai ya Washington kuhusu haki za binadamu.

Suala jingine ambalo ni muhimu ni kwamba, kwa nini ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa au ripoti nyinginezo kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran hazitaji maendeleo makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika eneo hili, au pale zinapotaja zinakuwa nakisi na zenye mapungufu au zinaambatanishwa na uchambuzi potovu na tafsiri zenye upendeleo? Hii ni pamoja na kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Iran haiwezi kulinganishwa na ile ya washirika wa nchi za Magharibi katika eneo hili la Magharibi mwa Asia, ambao wana rekodi nyeusi katika uwanja huu, kama vile Saudi Arabia. Hata hivyo Umoja wa Mataifa na washirika wa Kimagharibi wa utawala wa Saudia wanafumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo na wanataka tu kuzishutumu nchi zinazopinga tawala za Magharibi kama Iran, hivyo wanatumia suala hilo kama chombo cha propaganda na wenzo wa mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Tehran. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, haki za binadamu zimekuwa wenzo wa kisiasa kwa baadhi ya nchi za Magharibi kama Marekani, Canada na nchi kadhaa za Ulaya, huku kila siku walimwengu wakiendelea kushuhudia mifano mingi ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi hizo hizo.

Nosratollah Tajik, balozi wa zamani wa Iran nchini Jordan anasema: "Wamagharibi wanatumia mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kama vile iliyokuwa Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Haki za Kibinadamu la umoja huo kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa, ilhali katika nchi zao wenyewe, raia na wageni wanatendewa vibaya zaidi, lakini mashirika haya ya haki za binadamu yananyamaza kimya."

Nosratollah Tajik

Nukta nyingine muhimu ya kuashiriwa hapa ni  kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikishirikiana na jumuiya za kimataifa za haki za binadamu, na katika mkondo huu tunaweza kuashiria uanachama wa Iran katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu kama Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi, Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu na Mkataba wa Haki za Mtoto.     

Tags