Jun 23, 2022 07:47 UTC
  • Safari ya Lavrov mjini Tehran; ushirikiano wa muda mrefu kati ya Iran na Russia kwenye ajenda ya mazungumzo

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia aliwasili mjini Tehran Jumatano alasiri ambapo ameonana na kuzungumza na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Lavron ambaye yuko nchini kwa mwaliko rasmi wa waziri mwenzake wa Iran Hussein Amir-Abdollahian, anakusudia kujadiliana na viongozi wa Iran kuhusu mapatano ya ushirikiano wa muda mrefu na kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi wa pande mbili kwa kuzingatia ongezeko la vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia katika mgogoro wake na Ukraine.

Ushirikiano juu ya usalama wa kieneo unaozihusu nchi za Syria na Afghanistan ni miongoni mwa masuala yatakayopewa uzito katika mazungumzo hayo. Suala la mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni jambo jingine ambalo litajadiliwa katika mazungumzo ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu na viongozi wa Iran hapa mjini Tehran.

Katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika tarehe 3 Juni kati ya Lavrov na Amir- Abdollahian na kabla ya kupasishwa azimio la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Nishati ya Nyuklia ya IAEA dhidi ya Iran, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Russia alibainisha wazi upinzani wa nchi yake dhidi ya kupasishwa azimio hilo na kusisitiza kwamba ushirikiano wa Iran na wakala huo unapasa kutimia katika mkondo wa kiufundi tu.

Sergey Lavrov (kushoto) akilakiwa na Amir-Abdollahian mjini Tehran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zina maslahi ya pamoja kuhusiana na masuala ya pande mbili na hasa katika nyanja za kiuchumi, kijeshi, kiusalama na masuala ya kieneo na kimataifa yakiwemo ya kukabiliana na siasa za upande mmoja za madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

Kuhusu masuala ya kisiasa na usalama na kieneo na kimataifa, na hasa kadhia ya Syria na vile vile kukabiliana na kuenea satwa ya Marekani Asia Magharibi na maeneo mengine ya jadi yaliyo chini ya ushawishi wa Moscow, Russia ina msimamo unaofanana na wa Iran. Tehran na Moscow ziliimarisha pakubwa uhusiano wao mwezi Septemba 2015 katika kilele cha mgogoro wa Syria kwa ajili ya kupambana na ugaidi wa kimataifa, jambo ambalo liliimarisha sana usalama wa eneo.

Mbali na uhusiano wa kisiasa unaozidi kuimarika kati ya Russia na Iran, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara pia unaendelea kuongezeka kati ya pande hizo. Kiwango cha mabadilishano ya biashara kati ya nchi mbili mwaka uliopita wa 2021 kilifikia dola bilioni 4.5 na hii ni katika hali ambayo kiwango hicho kilikuwa ni cha dola bilioni 1.6 pekee mwaka 2019.

Mwezi Machi 2001 Iran na Russia zilitiliana saini mapatano ya miaka 20 ya kuimarisha ushirikiano wao na hivi sasa pia nchi hizo zinafuatilia kutia saini mapatano mapya ya muda mrefu kwa ajili ya kuimarisha mahusiano hayo na hasa katika uwanja wa uchumi.

Kuunganishwa reli ya Iran na Russia kupitia Turkmenistan na Kazakhstan, kubadilishana bidhaa zinazosafirishwa kwenda nchi nyingine pamoja na kuimarishwa shughuli za forodha katika maeneo ya kusini mwa Russia yanayopakana na Iran ni nyanja nyingine za ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi mbili na tayari zimekwishatia saini hati nne za maelewano kwa minajili ya kufikia lengo hilo na kukamilishwa miundomsingi ya usafiri na uchukuzi.

Safari ya karibuni ya Lavrov mjini Tehran

 

Katika hali ya hivi sasa kuimarishwa ushirikiano wa kibiashara wa muda mrefu kwa ajili ya kuondoa na kupunguza makali ya vikwazo ni jambo linalofuatiliwa kwa karibu na viongozi wa nchi mbili na bila shaka safari ya hivi sasa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia mjini Tehran imefanyika kwa lengo la kufanikisha jambo hilo.

Alexander Mariasov, balozi wa zamani wa Russia mjini Tehran anaamini kuhusu umuhimu wa uhusiano wa Russia na Iran kwamba: Suala la jamii ya kisasa iliyo nje ya Iran kukiri umuhimu wa Russia kwa Iran ikiwa mshirika muhimu katika kubuniwa mfumo wa kimataifa wa kambi kadhaa zenye nguvu na uungaji mkono wa Russia kwa juhudi za Iran za kujiunga na miungano kadhaa ya eneo la Eurasia kama vile Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni jambo linalothibitisha wazi kwamba uhusiano wa Russia na Iran utakuwa imara.