Jun 23, 2022 12:30 UTC
  • Lavrov: Russia inaunga mkono msimamo wa Iran katika kufufua JCPOA

Waziri wa mambo ya nje wa Russia amesema nchi yake inaunga mkono, bila kuongezwa wala kupunguzwa, yaliyomo katika msimamo wa Iran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Sergei Lavrov ametoa kauli hiyo leo katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mwenyeji wake, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian hapa mjini Tehran.

Akijibu suali la mwandishi wa shirika la habari la Iran Press kuhusu ushirikiano wa Iran na Russia katika kufikia makubaliano mazuri na ya kudumu; na kwa upande mwingine kuhusu hatua ya Marekani ya kuhalifu ahadi zake sambamba na kuiwekea Iran vikwazo vipya, Lavrov amesema: Si katika mazungumzo ya JCPOA pekee, bali katika kadhia nyingine zote, Marekani huwa inajali na kuzingatia masuala yake ya ndani tu.

Amir Abdollahian (kulia) na mgeni wake Sergei Lavrov

Waziri wa mambo ya nje wa Russia amefafanua kwa kusema: mwaka mmoja nyuma, Marekani ilitaka kutuvurumizia tuhuma kwamba sisi ndio tunaokwamisha mazungumzo ya Vienna, lakini pande zote zimekiri kwamba, ni Marekani peke yake ndio iliyokwamisha mchakato wa kufikia makubaliano.

Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Amir-Abdollahian amesema, Tehran inachukua hatua za kistratejia za kuzima athari za vikwazo kupitia pande mbili za serikali na diplomasia.

Amefafanua kwa kusema, sambamba na kuwepo vikwazo hivyo, kiwango cha mabadilishano ya kibiashara, kiuchumi, kielimu, kiulinzi na utalii na nchi jirani kimeongezeka pia.

Halikadhalika, Abdollahian amesisistiza kwamba, kuzima na kuhafifisha athari za vikwazo ni moja ya masuala yaliyoafikiwa kwa pamoja na Iran na Russia.../

Tags