Jun 24, 2022 01:18 UTC
  • Mahakama Iran yaitoza US faini ya bilioni 4.3 kwa mauaji ya wanasayansi wa nyuklia

Mahakama moja nchini Iran imeipata na hatia serikali ya Marekani na makumi ya taasisi na maafisa wa nchi hiyo kwa kuunga mkono na kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mauaji dhidi ya wanasayansi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.

Familia za wanasayansi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliouawa kigaidi, wajane watatu wa wanasayansi hao pamoja na mwanasayansi mmoja aliyejeruhiwa vibaya katika hujuma ya kigaidi ya Wazayuni wakishirikiana na Marekani, walifungua faili katika mahakama moja mjini Tehran, dhidi ya serikali ya Washington na taasisi na zilizokuwa ofisini wakati wa mauaji hayo ya kigaidi ya Israel.

Katika hukumu yake ya jana Alkhamisi, mahakama hiyo ya Tehran imeitaka Marekani ilipe fidia ya dola bilioni 4.3 inayojumuisha faini, kwa mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa taifa hili.

Mahakama hiyo imesema lengo la kesi hiyo ni kutaka kuzuia ukiukaji wa majukumu ya kimataifa na mienendo ya kiuadui katika medani ya kimataifa, kupitia kuunga mkono vitendo vya kigaidi vya utawala haramu wa Israel.

Waliopatikana na hatia katika kesi hiyo ni shakhsia na watu wa kawaida 37 wa Marekani, wakiwemo marais wa zamani wa nchi hiyo Barack Obama na Donald Trump. Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, Waziri wa Ulinzi wa zamani, Ashton Carter na mjumbe wa zamani wa masuala ya Iran, Brian Hook.

Familia ikimlilia mwanasayansi wa nyuklia wa Iran aliyeuawa shahidi

Wanasayansi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu wamekuwa wakilengwa na maajenti na majasusi wa nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuuawa. Kati ya mwaka 2010 na 2012, wanasayansi wanne wa nyuklia wa Iran, ambao ni Masoud Alimohammadi, Majid Shahriari, Darioush Rezaeinejad na Ahmadi Roshan waliuawa shahidi katika mashambulizi ambayo utawala khabithi wa Israel ulilaumiwa.

Aidha Novemba mwaka juzi 2020, Mohsen Fakhrizadeh, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Ubunifu wa Kiulinzi na Utafiti katika Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi katika shambulio jingine la kigaidi la Israel, huku Kanali Hassan Sayyad Khodaei akiuawa Mei 22 katika shambulio la hivi karibuni zaidi. 

 

 

Tags