Jun 24, 2022 08:07 UTC
  • Khatibzadeh: Uturuki isiyanyamazie madai ya kufarakanisha ya Wazayuni

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema, inatarajiwa kuwa Uturuki haitanyamazia kimya madai ya kufarakanisha yaliyotolewa na wazayuni.

Katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya na mwenzake wa Uturuki mjini Ankara, waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa kizayuni wa Israel amerudia tena madai yake kwamba eti Iran inataka kuwashambulia wazayuni ndani ya ardhi ya Uturuki.

Saeed Khatibzadeh amesema, tuhuma na madai yasiyo na msingi aliyotoa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa kizayuni Yair Lapid mjini Ankara katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ni kichekesho na ni mwendelezo wa sinario iliyopangwa tokea hapo kabla kwa lengo la kuharibu uhusiano wa nchi mbili za Kiislamu na pia ni sehemu ya njama ya Tel Aviv ya kuzibabaisha fikra za waliowengi ndani ya Uturuki na katika eneo kuhusiana na piganio tukufu la Palestina na vitendo vya kigaidi vya utawala huo unaoua watoto wadogo na kufanya hujuma na uharibifu.

Cavusoglu (kushoto) na Lapid

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran ameongeza kuwa, takriban tangu wiki moja nyuma, ilianzishwa operesheni ya vita vya kisaikolojia vilivyolenga kuvishughulisha vyombo vya habari na sinario ya kubuni kwa kutumia taarifa potofu na kwa lengo la kuandaa mazingira kwa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni kuibua mpango huo wa uzushi.

Khatibzadeh amebainisha kwa kusema, "nchi jirani yetu ya Uturuki inaelewa vyema ni kwa kiasi gani madai ya mjumbe huyo wa utawala mrongo na wa kigaidi wa kizayuni yasivyo na msingi wowote; na kianchotarajiwa ni kwamba haitanyamazia kimya madai hayo yanayolenga kuzusha mfarakano".../

 

Tags