Jun 24, 2022 11:50 UTC
  • Iran: Mataifa ya Asia Magharibi yanapaswa kuamua kuhusu mustakabali wa eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mataifa ya Asia Magharibi ndiyo yanayostahiki kuamua kuhusu mustakabali wa eneo hili la kistratijia.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad al Busaidi, ambapo wamejadiliana pia masuala ya kieneo na kimataifa na njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Amesema anaamini kuwa Tehran na Muscat zimejitolea kwa dhati kupanua na kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga tofauti, kama ilivyoafikiwa wakati wa safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Oman hivi karibuni.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alienda Oman na kupokewa rasmi na Sultan Haitham bin Tariq Aal Said wa nchi hiyo. Miongoni mwa matunda ya ziara hiyo rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Oman ni kutiwa saini hati 12 za kustawisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, Oman ina nafasi muhimu kwenye ustawi wa eneo la Asia Magharibi, hususan jitihada za Muscat za kutaka kuimarika usalama na amani katika eneo hilo, ikiwemo amani ya Yemen.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad al Busaidi amesema azma ya Iran kutaka kupanua uhusiano na nchi za eneo ni muhimu sana, na kusisitiza kuwa Muscat itajitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa hati ya pamoja ya maelewano kwa ajaili ya kupanua wigo wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tehran na Muscat inatekelezwa.

Tags