Jun 25, 2022 08:10 UTC
  • Iran yaanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Kituo cha Nyuklia cha Bushehr

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Kituo cha Nyuklia cha Bushehr (Bushehr-2) kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa nishati ya nyuklia nchini.

Oparesheni ya kuanza ujenzi wa tanuri nyuklia la Bushehr-2 ilianza Ijumaa katika sherehe iliyohudhuriwa na Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Mohammad Islami na pia mkuu wa mkoa wa Bushehr Ahmad Mohammad Zadeh.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bw. Islami amesema: "Kwa kuzingatia sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na irada ya Serikali ya Awamu ya 13 na hasa Rais Ebrahim Raiesi, tumejitahidi kuondoa vizingiti vyote katika ujenzi wa vituo vipya vya nyuklia vya kuzalisha umeme vya Busher 2 na 3.

Aidha Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema, wamefanya uchunguzi kuhusu vizingiti vyote katika ujenzi wa vituo hivyo viwili vipya vya nyuklia na sasa vimeweza kuondolewa,

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa, kinyume na madai ya maadui, miradi yake yote ya nyuklia inafanyika kwa malengo ya amani hasa ya kuzalisha nishati ya nyuklia ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. 

Awamu ya Kwanza ya Kituo cha Nyuklia cha Bushehr

Akizungumza katika  Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia ambayo huadhimishwa nchini Aprili 6,  Rais wa Jamhuri ya Kiislamu alizindua mafanikio mapya katika uga wa miradi ya nyuklia yenye malengo ya amani. Raisi alieleza furaha yake kutokana na mafankio ya vijana wasomi Wairani katika uga wa nyuklia na kusema, mafanikio hayo ni nembo ya kujiamini na kutegemea uwezo wa ndani ya nchi.

Rais wa Iran alisisitiza kuwa, Iran ina haki isiyopingika ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani. Aidha amesema wanasayansi Wairani wamechukua hatua nzuri za utafiti katika sekta ya nyuklia kwa malengo ya amani na hivyo serikali itaendelea kuwaunga mkono. Amesema, katu Iran haiwezi kusitisha shughuli zake za nyuklia.

Katika maonyesho hayo, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran lilizindua mpango wa kistratijia wa kuzalisha megawati 10,000 za umeme wa nyuklia kwa kutumia vituo vya nishati ya nyuklia vilivyoundwa kikamilifu ndani ya nchi.