Jun 25, 2022 10:17 UTC
  • Safari ya Borell Tehran; fundo la mazungumzo ya Vienna kufunguliwa au la?

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia kuhusu safari ya Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa Tehran.

Saeed Khatebzadeh jana alieleza kuwa, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya atakuwa na mazungumzo na Hossein Amir-Abdullahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na baadhi ya viongozi wengine wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia ya JCPOA na matukio ya kikanda na kimataifa.  

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya pia amethibitisha safari yake hapa Iran na kueleza kuwa, diplomasia ndio njia pekee ya kurejea katika utekelezaji kamili wa mapatano ya JCPOA. Tetesi kuhusu uwezekano wa Borrell kufanya ziara Tehran zilianza kusikika tangu kufanyika kikao cha waandishi wa habari na Amir Abdullahian akiwa na waziri mwenzake wa Russia Sergei Lavrov Alhamisi iliyopita; ambapo katika sehemu ya mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliashiria mashauriano mtawalia kati ya Ali Bagheri-Kani mkuu wa timu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo  ya Vienna na Enrique Mora Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya na pia mazungumzo kati yake na Joseph Borrell na kuahidi kwamba mashauriano kuhusu mapatano ya JCPOA yataanza siku chache zijazo.  

Ali Bagheri Kani na Enrique Mora katika moja ya mazungumzo yao Uswisi 

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna kuhusu kuindolea Iran vikwazo vya kidhalimu ambayo yalianza tangu Disemba 27 mwaka jana; tarehe 11 mwezi Machi mwaka huu yaliingia mapumzikoni kufuatia pendekezo lililotolewa na Josep Borrell, ambapo washiriki katika mazungumzo hayo walirejea katika miji mikuu ya nchi zao kwa ajili ya mashauriano zaidi ya kisiasa. Tokea wakati huo mwenendo wa mazungumzo hayo umetathminiwa katika hali ya kukaribia kugonga mwamba kwa sababu Marekani inaakhirisha kuchukua maamuzi ili kufidia hatua zake zilizo kinyume cha sheria mkabala wa Iran na mapatano ya JCPOA.  

Ni wazi kuwa, mazungumzo ya Vienna yamesimama kwa sababu, serikali ya Joe Biden licha ya kukosoa siasa zilizofeli za mashinikizo ya kiwango cha juu cha mtangulizi wake Trump yenyewe haikuwa tayari kurekebisha sera hizo na kuiondolea Iran vikwazo ipasavyo bali imekataa pia kuipatia Iran dhamana yenye itibari. Hii ni katika hali ambayo, Marekani inapasa kutoa hakikisho la kuidhaminia Iran maslahi yake kama sharti la kuhuisha mapatano ya JCPOA na kurejea Marekani katika mapatano hayo.

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; kile kinachoweza kuainisha kufikiwa mapatano ya kudumu ni kuondolewa kikamilifu vikwazo vya kidhulma dhidi ya Iran na kulindwa maslahi yake katika mapatano yatakayofikiwa; na ndio maana Iran imewasilisha pia mapendekezo na ubunifu wote wa lazima kwa minajili ya kufanikisha mazungumzo ya Vienna.  

Duru ya Nane ya mazungumzo ya Vienna 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wiki iliyopita alizungumza kwa simu na Josep Borrell; na akijibu ombi la kuendeleza mazungumzo alikumbusha kwamba: Tehran siku zote imekuwa ikiunga mkono mazungumzo ya mantiki na yenye natija hata hivyo kuna udharura upande wa pili nao kuachana na hatua zake za undumakuwili na zenye kukinzana katika uwanja huo.  

Mfano wa wazi wa hatua hizo za undumakuwili na zenye kukinzana za nchi za Magharibi tunaweza kutaja hatua isiyojenga ya karibuni ya Marekani na Troika ya Ulaya ya kupasisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyukilia (IAEA); hatua ambayo imekabiliwa na radiamali ya Iran. Iran imejibu hatua hiyo kwa kuzima kamera 27 zilizokuwa zmefungwa na wakala wa IAEA katika taasisi zake za nyuklia. Katika kuendelezwa hatua zake hizo haribifu, serikali ya Marekani miezi kadhaa iliyopita iliwawekea vikwazo vipya shakhsia na mashirika kadhaa ya Iran. 

Kuwepo mjini Tehran Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya huenda kukasaidia kuondoa vizuizi vinavyokwamisha mwenendo wa mazungumzo lakini kwa sharti kwamba serikali ya Marekani idhihirishe irada ya kweli ya kisiasa ya kurejea katika mapatano ya JCPOA. Enrique Mora mratibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA jana asubuhi alituma picha mtandaoni akiwa katika chakula cha jioni na Josep Borrell na Robert Marley Mkuu wa timu ya mazungumzo ya Marekani na kueleza kuwa, moja ya ajenda za mkutano wao ilikuwa ni kufufua mapatano ya JCPOA. Enrique Mora aidha amemnukuu Robert Marley na kuandika: "Marekani imedhamiria kurejea katika mapatano ya JCPOA."

Mapatano ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN 

Hakuna shaka kuwa, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya katika ziara yake mjini Tehran atakuwa amebeba ujumbe mpya wa Washington. Katika maashauriano yake na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itabainika wazi iwapo je Marekani ina dhamira ya kweli ya kurudi katika mapatano ya JCPOA na kubadili siasa zake mkabala wa Iran na mapatano hayo ya nyuklia au ingali ni kikwazo kikuu  katika kufikiwa natija mazungumzo ya Vienna kwa hatua zake za kupenda makuu na kushindwa kuchukua maamuzi ya kisiasa ya maana.