Jun 25, 2022 12:41 UTC
  • Amir-Abdollahian: Iran inataka iwe na uhusiano na dunia ulio na uwiyano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran inataka iwe na uhusiano na dunia ulio na uwiyano na kudumisha sambamba na kupanua uhusiano wake na bara la Ulaya.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell.

Amir-Abdollahian amefafanua kuwa, Iran inataka iwe na uhusiano na dunia wenye uwiano na kwamba kudumisha na kupanua uhusiano na bara la Ulaya ni katika vipaumbele vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha, waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema, kiwango cha uhusiano, hasa wa biashara, kati ya Iran na nchi za Ulaya hakiridhishi na akaongezea kwa kusema: "tunatumai kuwa zitapigwa hatua kupitia mwendelezo wa mazungumzo na makubaliano yaliyofikiwa leo".

Amir- Abdollahian amesisitiza pia kwamba kunufaika kikamilifu kiuchumi Iran ni miongoni mwa masuala muhimu na akafafanua kwa kusema: "tutajaribu, kupitia mazungumzo yatakayoanza tena karibuni, kuondoa vizuizi vilivyopo".

Mazungumzo baina ya ujumbe wa Iran na wa EU mjini Tehran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongezea kwa kusema: "tuna matumaini kwamba upande wa Marekani utachukua hatua za kiuwajibikaji kwa kuzingatia uhalisia wa mambo".

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkuu wa Sera za Nje wa EU Joseph Borrell amesema, kufikiwa makubaliano ni muhimu kwa ulimwengu.

Borrell ameongeza kuwa Iran ni nchi kubwa zaidi katika eneo na ina uwezo mkubwa katika uga wa nishati.

Mkuu wa Sera za Nje wa EU amesisitiza pia kwa kusema: "inapasa tuanzishe tena mazungumzo ya JCPOA, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran viondolewe na Iran inufaike kiuchumi".

Kwa mujibu wa Borrell, imepangwa kuwa mazungumzo hayo yaliyokuwa yamesita kwa karibu miezi mitatu yaanze tena.../

Tags