Jun 26, 2022 08:17 UTC
  • Raisi: Iran haitaondoka kwenye meza ya mazungumzo ya JCPOA

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Iran haitaondoka kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kuondolewa vikwazo.

Duru ya nane ya mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran huko Vienna iliyoanza Disemba 27, 2021, ilisitishwa Machi 11, 2022, kwa pendekezo la Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU) Joseph Borrell, na wapatanishi walirejea katika miji  mikuu ya nchi zao kwa mashauriano ya kisiasa. 

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye umedai kutumia njia za kidiplomasia kuhusiana na Iran na kwamba anafanya juhudi za kuirejesha nchi hiyo kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, hadi sasa haujachukua hatua zozote kuonyesha nia njema.

Karibu nchi zote zinazoshiriki katika mazungumzo hayo zinataka yakamilishwe haraka zaidi, lakini kufikiwa makubaliano ya mwisho kunasubiri maamuzi ya kisiasa ya Marekani kuhusu masuala machache yaliyosalia.

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU)

Katika mkondo huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, jana usiku (Jumamosi) katika hotuba yake kwa taifa aliashiria ziara ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya mjini Tehran na kusema kuwa, Iran haina nia ya kusitisha mazungumzo, lakini pia haitalegeza kamba katika misimamo yake. Amesema "Sera yetu ni kuondolewa vikwazo, na vikwazo hivi lazima viondolewe haraka, kwa sababu ni vya kidhalimu." 

Rais Ebrahim Raisi amesema kupasishwa azimio dhidi ya Iran katika Baraza la Magavana wa IAEA wakati wa mazungumzo ya kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran haikuwa hatua sahihi na kuongeza: Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umethibitisha mara kumi na tano kwamba hakuna mkengeuko wowote katika shughuli za nyuklia za Iran.

Tags