Iran yafanyia majaribio yaliyofana kombora la kubeba satalaiti la Zuljanah
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya majaribio yaliyofana ya kombora la Zuljanah la kubeba sataliti ambapo hili ni kombora la pili la utafiti kurushwa katika anga za mbali.
Akizungumza na waandishi habari, Msemaji wa Kitengo cha Anga za Mbali katika Wizara ya Ulinzi ya Iran amesema kombora hilo limerushwa katika anga za mbali kwa mafanikio. Ameongeza kuwa kombora au roketi ya satalaiti ya Zuljanah imeweza kuruka katika awamu tatu na limeweza kufikia malengo yaliyokusudiwa ya utafiti. Kombora la kwanza la kubeba satalaiti lilirushwa kwa mara ya kwanza katika anga za mbali mapema mwaka 2021 kwa mafanikio.
Akizungumza wakati huo baada ya kurushwa katika anga za mbali roketi hiyo ya kwanza ya Zuljanah, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri alisema "Roketi ya kubeba satalaiti ya Zuljanah ilirushwa kwa mafanikio katika awamu tatu na kufika katika eneo maalumu katika anga za mbali na katika hatua itakayofuata itabeba sataliti hadi katika anga za mbali zaidi."
Alisema Iran imeweza kupata mafanikio mazuri katika sekta ya uga wa makombora au maroketi ya kurusha satalaiti katika anga za mbali. Amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano wa karibu baina ya majeshi ya Iran, vyuo vikuu pamoja na mashirika ambayo msingi wake ni elimu.

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imefanikiwa kutuma satalaiti kadhaa katika anga za mbali kwa mafanikio. Aprili mwaka jana Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilifanikiwa kutuma katika anga za mbali sataliti ya kwanza ya Iran ya kijeshi.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Iran imejitahidi sana katika kuunda maroketi au makombora ya kubeba sataliti. Kabla ya kuunda maroketi hayo, Iran tayari ilikuwa imeshapata uwezo wa kuunda satalaiti na hivyo ikawa inahitaji chombo cha kurushia satalaiti hizo katika anga za mbali. Hali kadhalika Iran imeweza kuunda kituo cha ardhini cha kuwasiliana na satalaiti na kupokea taarifa zote zinazotumwa na sataliti hizo. Kwa msingi huo, Iran sasa imekamilisha mzunguko kamili unaohitajika katika uga wa sataliti.