Jun 27, 2022 10:39 UTC
  • Malengo ya safari ya Mustafa al Kadhimi mjini Tehran

Mustafa la Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq, baada ya kukutana na wakuu wa Saudi Arabia mjini Jeddah, moja kwa moja ameelekea Tehran Jumapili Juni 26 na kulakiwa rasmi na Rais Ebrahim Raeisi wa Iran.

Baada ya Rais Ebrahim Raeisi kuchukua rasmi hatamu za uongozi kama Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Moustafa la Kadhimi alikuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kusafiri nchini Iran na kukutana na rais wa serikali ya awamu ya 13 ya Iran mnamo Septemba 2021.

Hivi sasa miezi tisa baada ya safari hiyo, kwa mara nyingine, Mustafa al Kadhimi ametembelea Tehran na kufanya mazungumzo na Rais Raeisi. Ingawa masuala ya uhusiano wa nchi mbili yamejadiliwa katika mkutano wa Raeisi na Al Kadhimi, lakini inaonekana kuwa safari hiyo imekuwa na malengo mengine muhimu zaidi.

Baadhi ya duru zinadokeza kuwa, katika uga wa uhusiano wa pande mbili, viongozi hao wamejadili Iraq kununua gesi zaidi ya Iran, kadhia ya maji na mazingira na masuala mengine yanayohusiana na uchumi wa Iraq na hali kadhalika safari za ziara katika maeneo ya kidini ya nchi hizi mbili. Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari wa viongozi hao wawili, Rais Ebrahim Raeisi amesisistiza kuhusu kustawishwa uhusiano na Iraq katika fremu ya sera za ujirani mwema. Aidha amesema katika mkutano na Waziri Mkuu wa Iraq wamejadili uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara baina ya nchi hizo mbili na imeafikiwa kuwa uhusiano wa kiuchumi uimarishwe zaidi. Raeisi pia amezungumzia kuhusu kuunganishwa njia za reli za eneo la Shalamche la Iran na Basra nchini Iraq na imeafikiwa kuwa hatua za haraka zichukuliwe ili kufanikisha mradi huu.

Mbali na sisitizo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili, safari ya Al Kadhimi mjini Tehran inahusiana na masuala mengine matatu.

Al Kadhimi (kushoto) na Bin Salman

Kwanza ni kadhia ya uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uhusiano wa Iran na Saudi Arabia ulikatwa mwaka 2016. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Iraq imekuwa mwenyeji wa mazungumzo baina ya maafisa wa Iran na Saudia kwa lengo la kuhuisha uhusiano wa pande mbili na hadi sasa duru tano za mazungumzo zimeshafanyika. Inadokezwa kuwa hivi sasa Iran na Saudia zinakaribia kufikia mapatano.

Kabla ya kuwasili Tehran Jumapili, siku ya Jumamosi Al Kadhimi alikuwa mjini Jeddah ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia ambaye kimsingi hivi sasa ndiye mtawala wa nchi hiyo.

Ni kwa msingi huo ndio weledi wa mambo wanaamini kuwa, upatanishi baina ya Tehran na Riyadh ni lengo muhimu na asili la safari ya Al Kadhimi mjni Tehran. Ni kutokana na nukta hiyo ndio kanali ya televisheni ya Al Mayadeen ikatangaza kuwa sababu kuu ya safari ya Al Kadhimi katika miji ya Jeddah na Tehran ni kupatanisha pande mbili za Iran na Saudia ili zianzishe tena uhusiano wa kidiplomasia. Al Kadhimi anataraji kuwa, akifanikisha kuzipatanisha Iran na Saudia, basi hadhi ya Iraq itaimarika katika eneo la Asia Magharibi na itaweza kuonekana kuwa ni nchi yenye satwa na hivyo iwe miongoni mwa madola yenye taathira katika eneo kama vile Qatar, Oman na Kuwait.

Lengo la pili la safari ya Al Kadhimi mjini Tehran linahusiana na siasa za ndani ya Iraq katika kipindi hiki ambapo mrengo wa Sadr umejiuzulu katika bunge. Kujiuzulu mrengo huo kumeleta mabadiliko muhimu katika mligano wa nguvu katika bunge la Iraq hasa miongoni mwa mirengo ya kisiasa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Al Kadhimi analenga kupata uungaji mkono wa Iran na Saudi Arabia, madola mawili yenye taathira kieneo, ili  aweze kubakia katika cheo cha waziri mkuu.

Nukta ya mwisho kuhusu safari ya Al Kadhimi katika miji ya Jeddah na Tehran ni kuwa imefanyika huku rais Joe Biden wa Marekani akikaribia kuitembelea Saudi Arabia. Kuna uwezekano kuwa Al Kadhimi atashiriki katika kikao kitakachofanyika Jeddah baina ya Biden na viongozi kadhaa wa nchi za eneo. Hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa katika safari zake Tehran na Riyadh, Waziri Mkuu wa Iraq alikuwa anatekeleza jukumu la mabadilishano ya barua baina ya  wakuu wa Iran na Saudia.

Tags