Jun 27, 2022 11:25 UTC
  • Onyo la Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran kwa Israel

Kamanda mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuchukua hatua yoyote ya kichokozi katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, sera ya Israel ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na chokochoko zozote za utawala huo katika eneo zitakabiliwa na jibu mwafaka.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri ametoa inadhari hiyo leo Jumatatu hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na mwenzake wa Pakistan, Luteni Jenerali Nadim Reza Nishan.

Meja Jenerali Baqeri amesema utawala haramu wa Israel ndio mzizi wa shari na chimbuko la kuvurugika uthabiti katika eneo la Asia Magharibi. 

Kamanda wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, vikosi vya ulinzi vya taifa hili vimejiandaa kwa kiwango cha juu kukabiliana kitisho cha aina yoyote cha adui.

Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran ameuhutubu utawala wa Kizayuni kwa kusema: Kuruhusiwa Israel ndani ya Kamandi ya Majeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi CENTCOM, kuleta silaha na zana za kijeshi, na kushiriki katika luteka za kijeshi Asia Magharibi kutaibua hatari kubwa katika eneo hili la kistratajia.

Meja Baqeri ameeleza kuwa, Iran haitaruhusu vitisho hivyo, na bila shaka itatoa jibu mwafaka kwa chokochoko hizo.

Makamanda hao waandamizi wa majeshi ya Iran na Pakistan mbali na kuzungumzia masuala ya kieneo kama kushamiri ugaidi Afghanistan na mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen, lakini pia wamegusia kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kijeshi baina ya mataifa haya mawili jirani.

Tags