Jun 27, 2022 11:29 UTC
  • Mazungumzo ya kufufua JCPOA kufanyika katika Ghuba ya Uajemi

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema duru ijayo ya mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA itafanyika katika moja ya nchi za eneo hili la Asia Magharibi.

Katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari hii leo, Saeed Khatibzadeh amebainisha kuwa, "Mungu Akipenda, moja ya nchi za Ghuba ya Uajemi itakuwa mwenyeji wa mkutano huo, ambao utafanyika ndani ya siku chache zijazo wiki hii."

Mashirika ya habari ya al-Jazeera ya Qatar na Nour News ya Iran yameripoti kuwa, vikao vijavyo vya kufufua mapatano ya JCPOA yumkini vikafanyika mjini Doha.  

Khatibzadeh ameeleza bayana kuwa, mpira hivi sasa upo upande wa Marekani, na kwamba iwapo watatekeleza ahadi walizozitoa kwa mujibu wa Josep Borell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, basi kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano.

Ameongeza kuwa, vikao vijavyo vitajikita zaidi juu ya suala la kuondolewa taifa hili vikwazo haramu na vya kidhulma, akisisitiza kuwa vitafanyika katika sura ya mikutano ya Vienna. Amesema Iran haitafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, na kwamba pande mbili zitawasiliana kwa njia isiyo ya moja kwa moja kama ilivyokuwa huko Vienna.

Mkutano wa nyuma wa Vienna

Kwengineko katika kikao hicho na waandishi wa habari hapa mjini Tehran, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema Marekani ndiyo mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kadhalika Khatibzadeh ametumia jukwaa hilo kutangaza kuwa muda wake wa kuwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran umemalizika, na nafasi yake inachukuliwa na Naser Kanani.

Tags