Jun 28, 2022 02:45 UTC
  • Indhari ya Waziri wa Usalama wa Iran: Magaidi hawatabakia salama

Waziri wa Usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema magaidi wenye makao yao Albania hawatabakia salama kutokana na moto wa ulipizaji kisasi wa jinai walizotenda.

Kundi la kigaidi la Munafikina (MKO) limehusika katika mauaji ya Wairani zaidi ya elfu 17, wakiwemo wabunge, maafisa wa ngazi za juu wa kiserikali na kijeshi, raia wa kawaida wasio na hatia na raia wa kigeni.

Mauaji hayo ya kigaidi yalitekelezwa kwa kuratibiwa na yalijumuisha mauaji ya ufyatuaji risasi, utegaji mabomu, utekaji nyara na utesaji n.k. Hujuma hizo za kigaidi na kihaini ni sehemu tu ya jinai nyingi za kigaidi za makundi ya kigaidi dhidi ya watu wa Iran wa matabaka mbali mbali ya jamii.

Magaidi wa kikundi cha munafikina kila mwaka huandaa mikutano ya hadhara Ulaya na Marekani kwa idhini ya nchi hizo. Hivi karibuni pia  Mike Pence, aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani wakati wa urais wa Donald Trump alishiriki katika kikao cha magaidi MKO ambacho kilifanyika katika makao yao nchini Albania. Katika mkutano huo Pence alikutana na kinara wa magadii wa MKO Maryam Rajavi. Mwaka jana pia Pence alishiriki kikao kingine cha kundi hilo la kigaidi la MKO.

Kazem Gharibabadi, Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu kushiriki Mike Pence katika kikao hicho cha magaidi wa MKO na kusema: "Mkutano wa Mike Pence na magaidi wa kundi la munafikina ni ushahidi wa wazi kuwa utawala wa Marekani unaunga mkono ugaidi. Marekani inawatakia mabaya watu wa Iran kwani Wairani 17,000 wameuawa na kijikundi hiki kinachofyonza damu na chenye sifa chafu.

Tokea siku za awali kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kuvurugika mahesabu ya madola ye kibeberu na kiistikbari duniani, Iran ilisuhudia kilele cha uhasama na chuki ya maadui na vibaraka wao wakiwemo wafuasi wa kundi la munafikiana au MKO.

Kazem Gharibabadi, Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran

Katika kipindi cha kuanzia 31 Machi 1983 hadi 20 Februari 1984 magaidi wa MKO walitekeleza mauaji ya umati ya Wairani 4583. Kundi la MKO lilikiri kuhusika na jinai hizo.

Baada ya kutimuliwa Iran, magaidi wa MKO  walielekea Iraq kwa idhini ya utawala wa Baath wa Iraq wakati huo ambapo mtawala wa wakati huo, Saddam, binafsi aliwakaribisha katika nchi hiyo. Magaidi hao walishirikiana na utawala wa Iraq kwa muda mrefu katika masuala ya ujasusi dhidi ya Iran ambapo wakiwa katika nchi hiyo walitekeleza oparesheni kadhaa za kigaidi dhidi ya Iran. Oparesheni ya Chelcheragh ilikuwa oparesheni mashuhuri zaidi ya magaidi wa MKO dhidi ya Iran lakini ilifeli kutokana na pigo kali ambalo walipata kutoka kwa majeshi shupavu ya Iran.

Magaidi hao waliendelea kubakia Iraq hadi wakati wa mwisho wa utawala wa Saddam na baada ya Marekani kuivamia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu ambapo magaidi hao walipewa hifadhi katika kambi maalumu nchini Iraq. Hata hivyo baada ya serikali mpya ya Iraq chini ya Waziri Mkuu Nouri al Maliki kuingia madarakani nchini, magaidi wa MKO walipewa makataa kuondoka Iraq haraka iwezekanavyo. Kwa msingi huo baada ya miaka kadhaa ya mvutano, hatimaye magaidi hao wa MKO walipelekewa Albania ambayo ni kijiinchi kidogo kisichojulikana na wengi Ulaya Mashariki. Uwepo wa magaidi hao huko Albania unafadhiliwa na Marekani. Kundi la munafikina linachukiwa sana nchini Iran kiasi kwamba hata ripoti rasmi za Marekani zinakiri kuwa kundi hilo haliungwi mkono na Wairani.

Katika kuendeleza uhasama wake dhidi ya Iran, utawala wa Kizayuni wa Israel umemkaribisha kinara wa MKO Maryam Rajavi mjini Tel Aviv ambapo amekutana na wakuu wa utawala wa huo. Hilo si la kushangaza kwani utambulisho wa Israel ni ugaidi. Utawala wa Kizayuni wenywe umehusika katika mauaji ya kigaidi ya idadi kubwa ya Wairani wakiwemo wanasayansi na wasomi bingwa na hivyo kundi la munafikana halina tofauti na utawala wa Kizayuni katika kutumia mbinu za ugaidi katika sera zao.

Hayo yanajiri wakati ambao dunia inahitaji azma imara kukabiliana na ugaidi. Hata hivyo ushahidi na sera za kimataifa zinaonyesha hakuna irada imara ya kukabiliana na uovu huo na mfano wa wazi ni namna ambavyo wakuu wa nchi za Magharibi na muitifaki wao mkuu, yaani utawala haramu wa Israel, ni waungaji mkono wakuu wa kundi la kigaidi la mko.

Pamoja na kuwepo kila aina ya hujuma za kundi la kigaidi la munafikina dhidi ya Iran, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko imara na inafuatilia kikamilifu taarifa zote za kiusalama Asia Magharibi na hivi sasa Iran ni moja ya nchi salama na yenye uthabiti zaidi katika eneo na kwa msingi huo inachukua hatua kali kukabiliana na njama zozote za kundi la kigaidi la munafikina.

Ni kwa msingi huo ndio Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran, Sayyid Ismail Khatib akatoa onyo kali kwa kundi la kigaidi la munafikina na waungaji mkono wake wa Magharibi na Kizayuni kwamba: "Magaidi walio na sifa chafu wanaoishi Albania kamwe hawatakuwa mbali na moto wa ulipizaji kisasi wa mashahidi 12,000 waliopoteza maisha kutokana na jinai zao. " Ameongeza kuwa ulipizaji kisasi huo utawafikia tu hata kama wanajikurubisha na wanatumiwa na vinara wa ugaidi rasmi wa kiserikali kama utawala wa Trump, Mike Pence na Pompeo.

Tags