Jun 28, 2022 03:16 UTC
  • Iran: Utawala wa Kizayuni ndio adui namba moja wa umma wa Kiislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni ndio adui nambari moja wa ulimwengu wa Kiislamu.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumatatu mjini Ankara katika kikao na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, ambapo pia amelipongeza taifa la Uturuki kwa kuunga mkono ukombozi wa Palestina.

Amir Abdollahian amesema bayana kuwa: Tunautazama utawala bandia wa Israel kama adui mkubwa zaidi wa umma wa Kiislamu.

Ameongeza kwa kusema kuwa, "Tuna uhakika kuwa Uturuki haijawahi kujiweka mbali na kadhia ya kuliunga mkono taifa la Palestina, na vile vile ukombozi wa mji wa al-Quds na Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameashiria safari ya Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya mjini Tehran na kueleza kuwa, anatumai kuwa, duru ijayo ya mazungumzo ya Iran na upande wa pili wa JCPOA itazaa matunda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipokutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa kuamkia leo alikutana pia na kufanya mazungumzo na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan.

Amir-Abdollahian ambaye yupo Ankara kufuatia mwaliko wa mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu anatazamiwa kwenda Turkmenistan kushiriki mkutano wa ngazi ya mawaziri wa nchi zinazolizunguka Bahari ya Caspian.

Tags