Jun 28, 2022 08:06 UTC
  • Bagheri Kani aelekea Doha kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya JCPOA

Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA anaelekea Doha, mji mkuu wa Qatar kwa ajili kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu.

Ali Bagheri Kani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameenda Doha leo Jumanne, siku chache baada ya Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Joseph Borrell kuja hapa Tehran kwa ajili ya kujaribu kutanzua kitendawili cha kukwama mazungumzo ya JCPOA huko Vienna nchini Austria.

Huko nyuma, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran alisitiza kuwa, siasa za kiistratijia za Jamhuri ya Kiislamu ni kufelisha vikwazo vya maadui.

Kanali ya Press TV ya Iran imeripoti kuwa, Robert Malley, Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran jana Jumatatu alielekea Qatar, kwa ajili ya kushiriki mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Tehran, juu ya njia za kuhuisha mapatano hayo ya nyuklia.

Robert Malley

Akiwa hapa Tehran, Mkuu wa Sera za Nje wa EU alisisitiza kuwa: "inapasa tuanzishe tena mazungumzo ya JCPOA, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran viondolewe na Iran inufaike kiuchumi".

Mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea vikwazo haramu taifa la Iran yalikuwa yamesita kwa karibu miezi mitatu, baada ya kufanyika duru kadhaa kati ya Iran na kundi la 4+1.

 

Tags