Jun 28, 2022 14:09 UTC
  • Ukosoaji wa Iran kwa jamii ya kimataifa kwa kutowajibika ipasavyo katika vita dhidi ya dawa za kulevya

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi na taasisi za kimataifa duniani haziwajibiki katika vita dhidi ya mihadarati kwa mujibu wa majukumu yao.

Sayyid Ebrahim Raisi ambaye juzi Jumapili alishiriki katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Mihadarati  alipongeza mchango mkubwa wa Wairani 3,800 waliouawa shahidi na wengine elfu 12 kuwa vilema katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na wakati huo huo amekosoa kutowajibika nchi mbalimbali duniani hasa Umoja wa Mataifa katika vita ya kutokomeza madawa ya kulevya.  

Tarehe 17 hadi 26 mwezi Juni mwaka 1987 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitisha Mkutano wa Kimataifa wa Kupambana na Uraibu na Biashara ya Madawa ya Kulevya katika mji wa Vienna. Nchi zilizohudhuria mkutano huo zilisaini hati iliyopewa jina la C.M.O ambayo iliainisha sera ya pamoja inayobainisha hatua zinazohitajika kuchukuliwa na nchi washiriki ili kudhibiti madawa ya kulevya. Hati hiyo ilizitaka nchi hizo kuchukua hatua kali kimataifa katika vita dhidi ya madawa ya kulevya. 

Pamoja na kuwa suala la kuzalisha na biashara ya mihadarati ni kadhia inayoihusu dunia nzima na taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zimeahidi kutoa uungaji mkono wa pande zote katika vita dhidi ya jambo hilo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaonekana takriban ikibakia peke yake katika mapambano hayo huku taasisi za kimataifa, kama Umoja wa Mataifa, zikipunguza uwajibikaji wao hata ule wa misaada yao midogo kwa Iran na kutosheka kwa kupongeza juhudi zake kwa maneno matupu. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kuwa jirani na nchi ya Afghanistan ambayo inahesabiwa kuwa mzalishaji mkubwa wa madawa ya kulevya duniani, siku zote imekuwa ikikabiliwa na magenge ya wafanya biashara haramu ya madawa hayo kuelekea katika nchi za Ulaya. Ndio maana Umoja wa Mataifa mwaka 2019 ulitangaza kuwa Iran imekamata asilimia 90 ya afyuni, asilimia 70 ya morphine, na asilimia 20 ya heroini ya dunia nzima. 

Hii ni katika hali ambayo, licha Iran kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya lakini takriban hakuna msaada wowote mkubwa inaoupata katika uwanja huo. Hadi sasa maelfu ya askari wa Iran wameuawa shahidi na maelfu ya wengine wamejeruhiwa katika mapambano dhidi ya biashara ya mihadarati. Iran aidha kila mwaka hutumia karibu dola milioni 350 kwa ajili ya kupambana na madawa ya kulevya huku ikikabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi.  

Ukweli ni kuwa, hakuna nchi ambayo inaweza peke yeke kundesha vita dhidi ya janga hilo na kutoa gharama zake zote; kwa msingi huo kuna ulazima nchi zote na taasisi za kimataifa ziwajibike ipasavyo. Hata hivyo hadi sasa zimeshindwa kuwajibika katika uwanja huo. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameashiria suala hili na kukumbusha kuwa: Swali langu kwa Umoja wa Mataifa ni kwamba: Je utendaji wa umoja huu katika vita dhidi ya mihadarati unalingana na nafasi, ukubwa, na hadhi yake? Je, ofisi moja ya kupambana ya mihadarati ndani ya Umoja wa Mataifa inatosha kweli kufanikisha jambo hilo? 

Rais Ebrahim Raisi

Nukta nyingine muhimu katika uwanja huu ni  kuongezeka uzalishaji wa madawa ya kulevya huko Afghanistan baada ya kuweko nchini humo vikozi vamizi vya Marekani na nchi nyingine wanachama wa muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi (NATO). Mwaka 2000 uzalishaji wote wa madawa ya kulevya nchini Afghanistan ulikuwa karibu tani 200; na mwaka 2018 kiwango hicho kilifikia tani elfu 9, yaani uzalishaji na uvunaji wa mihadarati uliongezeka mara 45. Ni wazi kuwa uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan umesababisha kuongezeka umaskini, maafa na hasara mbalimbali, ukosefu wa ajira na ufisadi nchini humo; mambo ambayo yanatajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za kuongezeka uzalishaji na madawa ya kulevya huko Afghanistan.  Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, maeneo ya mashamba ya dawa za kulevya huko Afghanistan yaliongezeka mara kumi baada ya nchi hiyo kuvamiwa na kukaliwa na kkaliwsa kwa mabavu na Marekani.

Uzalisha na biashara ya madawa ya kulevya duniani inaonyesha kuwa hakuna irada yoyote ya dhati kimataifa ya kupambana ipasavyo dhidi ya biashara hiyo; na si nchi au taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zinazotekeleza majukumu yao katika uwanja huo. Hali hii inazidisha mazingira ya sasa au hata kuyafanya mabaya zaidi. Kwa hiyo, kuna udharura  kwa jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake katika vita vya pande zote dhidi ya kilimo, uzalishaji, uuzaji na matumizi ya mihadarati ili kujinasua katika janga kubwa linaloitatiza dunia sasa. 

Kama alivyoeleza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaonekana kuwa kuna udhaifu mkubwa katika kuchukua maamuzi yanayohitaji ya kimataifa katika vita dhidi ya madawa ya kulevya; na hali haitaboreka hadi udhaifu huo utakapoondolewa.