Jun 29, 2022 07:34 UTC
  • Mazungumzo ya Doha; fursa kwa Marekani ya kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA

Mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani kuhusu uondoaji vikwazo yalianza jana Jumanne katika mji mkuu wa Qatar, Doha kwa kupitia kwa Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya.

Baada ya safari ya Mkuu wa Sera za Nje wa EU Josep Borrell hapa mjini Tehran na mazungumzo aliyofanya na maafisa wa Iran ilitangazwa kuwa, kulingana na uamuzi uliochukuliwa na Iran na Marekani, mazungumzo kuhusu kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa Iran yataanza tena siku ya Jumanne.

Ali Baqeri Kani, kiongozi mwandamizi wa timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za nje wa Umoja wa Ulaya, ambaye pia ni mratibu wa mazungumzo ya JCPOA walikutana na kufanya mazungumzo hapo jana huko mjini Doha.

Ali Baqeri Kani (kulia) na Enrique Mora

Naye Robert Malley, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, ambaye ameelekea huko Doha kwa madhumuni hayo hayo, yeye amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdurahman Al Thani.

Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya wawakilishi wa Iran na wa nchi zinazounda kundi la 4+1, ambazo ni Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu uondoaji vikwazo yalianza Desemba 2021 mjini Vienna na yakasimamishwa mwezi Machi 2022 kwa pendekezo la Josep Borrell. Kuanzia wakati huo, baadhi ya nchi ikiwemo Qatar, zimefanya juhudi mbalimbali za upatanishi na kufikisha jumbe za mashauriano kwa kila upande. Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetoa taarifa kuhusu mazungumzo ya uondoaji vikwazo na kutangaza kwamba: matumaini yaliyopo ni kuwa, mazungumzo hayo yatamalizika kwa kuwa na tija na matokeo chanya.

Pamoja na hayo, kuanza tena mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani hakumaanishi kwamba makubaliano ya JCPOA yanakaribia kufufuliwa upya, kwa sababu mwafaka wowote wa sasa unafungamana na maamuzi ya kisiasa ya Marekani; na kusainiwa makubaliano hayo kunategemea na kuondolewa vikwazo na kuipatia Iran dhamana na hakikisho la uhakika. Ukweli ni kwamba, kitu kinachoweza kutoa hakikisho la kufikiwa makubaliano thabiti na endelevu, ni kuondolewa kivitendo vikwazo na kudhaminiwa Iran maslahi yake. Na ndio maana Tehran imetoa mapendekezo na ubunifu unaopasa kufanyiwa kazi ili kuweza kufikia mwafaka katika mazungumzo ya sasa.

Hayo yanajiri wakati mazungumzo ya Doha yakiwa yanakaribia kuanza, Ikulu ya Marekani White House ilitoa kauli ya kujaribu kujivua masuulia na wajibu ilionao na kudai kwamba, hatima ya mazungumzo hayo inategemea maamuzi ya Iran. Pasi na kuashiria chochote kuhusu nafasi ya nchi yake katika ukiukaji wa makubaliano ya JCPOA, Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa Joe Biden amejaribu kwa mara nyingine kuitupia mpira Iran, huku akirudia tena madai ya kila mara ya Washington kwa kusema: "kuhusu Iran inapasa niseme kwamba, mtazamo wa Marekani umekuwa wazi tangu muda mrefu nyuma, kwa maana kwamba, sisi tumedhamiria kuizuia Iran isimiliki silaha za nyuklia".

Hapana shaka kuwa, kutolewa kauli kama hizo na maafisa wa Marekani kunazidi tu kuipa nguvu hoja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutaka lazima yawepo makubaliano thabiti na endelevu ili mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaweze kutekelezwa kikamilifu; na sababu ni kwamba, serikali za Marekani, ziwe za Warepublican au Wademocrat zimeshaonyesha kuwa katika utekelezaji, zinafuata takriban siasa na sera zinazofanana dhidi ya Iran. Kusita kwa mazungumzo ya Vienna pia, sababu yake ni kwamba kinyume na msimamo wake wa awali wa kukosoa sera iliyogonga mwamba ya Trump ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran, serikali ya Joe Biden nayo pia baada ya kuingia madarakani haikuwa tayari kubadilisha sera hiyo kwa kukataa kuondoa vikwazo na kuipatia Tehran hakikisho lenye dhamana na uhakika.

Kwa maana hiyo, mazungumzo ya hivi sasa ya mjini Doha ni fursa nyingine kwa serikali ya Marekani ya kuonyesha irada ya kisiasa inayohitajika kwa ajili ya kufikia makubaliano; irada ambayo kupatikana kwake kunahitaji kuangalia mambo kwa uhalisia wake, kuchukua hatua za kujenga hali ya kuaminiana na vilevile kuachana na tabia ya kuibua matakwa mapya na potofu yasiyo na uhusiano wowote na JCPOA.

Saeed Khatibzadeh

Siku ya Jumatatu, aliyekuwa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh alisema yafuatayo kuhusu mazungumzo ya Doha: "Ninaweza kutihibitisha kuwa mwafaka umefikiwa kwa upande wa maudhui zote mbili za namna mazungumzo yatakavyokuwa na yatakayojadiliwa ndani yake, lakini kwamba katika utekelezaji Wamarekani wataweza kuonyesha kuwa wanaachana na mirathi ya Trump na wanataka kuwa watu wawajibikaji, hilo itapasa tusubiri".../