Jun 29, 2022 14:00 UTC
  • Raisi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua Bahari ya Kaspi kuwa bahari ya amani na urafiki

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika Mkutano wa Sita wa Nchi za Pwani mwa Bahari ya Kaspi kuwa: Iran inaitambua bahari hiyo kuwa ni bahari ya amani na urafiki na kiunganishi cha watu wa eneo hili. Sayyid Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa Iran iko tayari kwa ajili ya ushirikiano wa pande zote kwa msingi wa kuheshimiana na kuchunga maslahi ya pamoja.

Akihutubia Mkutano wa 6 wa wakuu wa nchi za kandokando ya Bahari ya Kaspi huko Ashgabat leo (Jumatano), Rais wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi amesema: "Tumeweka misingi ya kisheria inayofaa ya ushirikiano na kufaidika na tunu za bahari hii kwa kuandaa hati kadhaa, na mafanikio haya yote ni matokeo ya juhudi, umaizi, kuona mbali na kuzingatia haki na maslahi ya pande zote za nchi zetu."

Rais Ebrahim Raisi ametilia mkazo ushirikiano wa nchi tano za kandokando ya Bahari ya Caspi na kuepuka hatua za upande mmoja, kutegemea uwezo uliopo na kupanua ushirikiano, ili kulifanya eneo la bahari hiyo kuwa "eneo la amani na urafiki".

Rais wa Iran pia amesema: "Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kutayarisha mazingira mazuri ya usafirishaji wa nchi za kandokando na Bahari ya Kaspi kuelekea katika maeneo mengine ya dunia hususan bandari za Iran katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman kwa kuzingatia nafasi yake nzuri ya kijiografia na miundombinu inayofaa."

Rais Ebrahim Raisi akihutubia mkutano wa Ashgabat

Mbali na kushiriki na kuhutubia mkutano wa Turkmenistan, Rais wa Iran atakutana na kufanya mazungumzo na marais wa nchi wanaoshiriki katika mkutano huo.

Mkutano wa 6 wa Nchi za Pambizoni mwa Bahari ya Kaspi unafanyika leo huko Ashgabat mji mkuu wa Turkmenistan kwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi tano za kandokando ya bahari hiyo yaani Iran, Russia, Turkmenistan, Kazakhistan na Jamhuri ya Azerbaijan.