Jun 30, 2022 02:54 UTC
  • Raisi: Uwepo wa utawala wa Kizayuni unadhoofisha usalama wa eneo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaibua taharuki na kudhoofisha usalama wa eneo hili la Asia Magharibi.

Rais wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatano katika kikao na mwenzake wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, pambizoni mwa Mkutano wa 6 wa Nchi Zinazopakana na Bahari ya Kaspi huko Ashgabat, mji mkuu wa Turkmenistan.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, usalama wa eneo hili utaimarishwa tu kupitia ushirikiano wa nchi za eneo, na mataifa yanayopakana na Bahari ya Kaspi.

Kadhalika Sayyid Raisi amebainisha kuwa, kuna fursa na uwezekano wa kupanua zaidi uhusiano wa Tehran na Baku katika nyuga za siasa, uchumi, biashara, na utamaduni.

Marais wa Iran na Russia pambizoni mwa mkutano wa Ashgabat

Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev kwa upande wake, sanjari na kuashiria mkutano wa mwisho uliofanyika kati yake na Rais Raisi wa Iran mnamo Novemba mwaka jana pambizoni mwa Mkutano wa Ushirikiano wa Uchumi mjini Ashgabat, amesema anatumai mazungumzo yake ya jana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu yataandaa mazingira ya kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran hiyo jana Jumatano mbali na kukutana na mwenzake wa Jamhuri ya Azerbaijan, alikutana pia na kufanya mazungumzo na marais wa nchi nyingine za Pwani ya Bahari ya Kaspi, ambazo ni Russia, Turkmenistan, na Kazakhistan.

Tags