Jun 30, 2022 08:15 UTC
  • Mazungumzo ya Doha yamalizika, pande husika zaahidi kudumisha mawasiliano

Mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani kuhusu uondoaji vikwazo yaliyoanza juzi Jumanne katika mji mkuu wa Qatar, Doha yamemalizika; huku pande mbili zikisema kuwa zitaendelea kuwasiliana juu ya marhala zijazo za mazungumzo hayo.

Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ndiye aliyekuwa mpatanishi kwenye mazungumzo hayo, baina ya kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, Ali Bagheri Kani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Robert Malley, Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Nasser Kan'ani ameandika katika ukurasa wa Twitter kuwa: Katika kuendelea na mchakato wa mazungumzo ya kuondoa vikwazo, mazungumzo ya kina yamefanyika mjini Doha siku ya Jumanne na Jumatano, kwa upatanishi wa Enrique Mora.

Kan'ani ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekabidhi mitazamo na mapandekezo yake, huku upande wa pili pia ukiwasilisha maoni yake. 

Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ameashiria mazungumzo hayo katika ujumbe wake wa Twitter na kusema: Tutaendelea kufanya kazi hata kwa udharura zaidi, ili kuyarejesha katika mkondo mapatano muhimu ya kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia na kuimarisha uthabiti katika eneo.

Hossein Amir-Abdollahia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran (kulia) na mwenzake wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani

Wakati huohuo, Hossein Amir-Abdollahia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani wamewasiliana kwa njia ya simu na wakajdili juu ya mazungumzo hayo ya Doha ya kuondolewa Tehran vikwazo haramu.

Aidha wawili hao wamegusia masuala ya kieneo na kimataifa, sambamba na uhusiano wa pande mbili wa Doha na Tehran. Maelezo zaidi juu ya mazungumzo ya wanadiplomasia hao wa Iran na Qatar hayajatolewa.

Naye Mohammad Marandi, mshauri wa Iran kwa timu ya mazungumzo ya Iran amekadhibisha ripoti kwamba mazungumzo ya Doha yamegonga mwamba na kusisitiza kuwa: Hakukuwa na matarajio yoyote kwamba mazungumzo hayo yamepelekea kufikiwa makubaliano ndani ya siku chache. Amesisitiza kuwa mazungumzo hayo yataendelea.

Tags