Jul 01, 2022 10:13 UTC
  • Iran iko tayari kusaidia utatuzi wa kidiplomasia wa mzozo wa Ukraine

Iran imesisitiza dhamira yake ya kuchangia katika utatuzi wa kidiplomasia wa mzozo unaotokota nchini Ukraine, ambao sasa unaingia mwezi wa tano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba  ameashiria msimamo wa Iran wa kupinga vita na kusisitiza juu ya kutatuliwa mgogoro huo kwa njia za kidiplomasia.

"Tumesema tangu awali kwamba wakati tunazingatia sababu ya mzozo, tunapinga vita na hatuzingatii vita kuwa suluhisho linalofaa la kutatua masuala," mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema.

Amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Ukraine umeegemezwa kwenye msingi wa urafiki, heshima, manufaa na ushirikiano wa pande zote katika miongo mitatu iliyopita na kueleza utayarifu wa kushirikiana [na Ukraine] ndani ya mfumo wa makubaliano ya ufunguzi wa ukanda wa Bahari Nyeusi ili kusafirisha bidhaa za nafaka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ametoa mwaliko kwa mwenzake wa Ukraine kutembelea Tehran.

Kuleba, kwa upande wake, ameshukuru msimamo wa Iran dhidi ya vita na kusisitiza kwamba serikali ya Ukraine itakaribisha msaada wowote wa kisiasa katika kumaliza mgogoro huo.

Pia ameelezea utayarifu wa Kiev  wa kupanua uhusiano wa pande mbili na Iran, ikiwa ni pamoja na katika nyanja za kilimo na nafaka.

Mwanadiplomasia mkuu wa Kiev pia amejadili maendeleo ya hivi punde ya vita katika nchi yake na akamshukuru Amir-Abdollahian kwa nia ya Tehran ya kuchangia katika kutatua mzozo huo na akamkaribisha kutembelea Kiev.

Hayo yamejiri huku mkuu wa NATO inayoongozwa na Marekani akionya kwamba mzozo wa sasa nchini Ukraine unaweza kugeuka na kuwa vita visivyozuilika kati ya muungano huo wa kijeshi wa Magharibi na Russia.

 

Tags