Jul 02, 2022 06:00 UTC
  • Sisitizo la kuwepo mabadilishano huru ya kifedha baina ya Iran na Russia, bila kutegemea Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mabadilishano ya kifedha kati ya Iran na Russia yanapaswa kuzidishwa bila kutegemea mfumo wa miamala ya kifedha wa nchi za Magharibi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais Vladimir Putin wa Russia kando ya mkutano wa kilele wa Bahari ya Kaspi huko Turkmenistan na kuongeza kuwa: "Mfumo huo huru wa kifedha utazuia ushawishi na mashinikizo ya nchi nyingine."

Iran na Russia ambazo ni miongoni mwa wapinzani wa sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika uga wa kimataifa zinakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi hususan Marekani kwa visingizio mbalimbali kama miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia na mgogoro wa Ukraine. Hata hivyo vikwazo, mashinikizo na vitisho vya Marekani na washirika wake vimekuwa na matokeo ya kinyumenyume; kwa sababu mbali na uhusiano unaozidi kuimarika kila uchao baina ya Iran na Russia, uhusiano wa kibiashara na kiuchumi wa pande hizo mbili pia unastawi siku baada ya nyingine. Kiwango cha biashara baina ya Iran na Russia mwaka uliopita wa 2021 kiliongezeka kwa asilimia 80 na kufikia karibu dola bilioni nne kwa mwaka, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya biashara ya nchi hizi mbili. 

Kwa sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zinashauriana kuhusu uwezekano wa kutumia mfumo wa miamala ya kifedha tofauti kabisa na ule wa Swift kwa lengo la kusahilisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara. Benki Kuu ya Iran pia imetangaza kuwa, inafanya maandalizi ya kuanza kutumia sarafu ya Russia, Ruble na ya Iran, Toman katika miamala yao ya kibiashara. 

Wakati huo huo Russia imependekeza kwamba nchi wanachama katika jumuiya ya BRICS ambazo ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini zitumie mfumo wao mmoja wa fedha katika miamala ya kibiashara. Iran pia imeomba uanachama katika jumuiya hiyo, na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia, Sergei Lavrov amesisitiza kuwa, Iran ina hadhi ya kuwa mwanachama katika kundi la BRICS na kwamba kuwepo Iran katika jumuiya hiyo kuna thamani kubwa.

Sergei Lavrov

Kwa sasa suala la kustawishwa ushirikiano wa kibiashara, kupanua ushirikiano wa muda mrefu, kuondolewa baadhi ya vizingiti na juhudi za kubatilisha vikwazo ndio ajenda kuu ya viongozi wa Iran na Russia. Ushirikiano wa pande mbili katika sekta ya nishati, kuunganisha njia za reli za Iran na Russia kupitia Turkmenistan na Kazakhstan, upanuzi wa bidhaa za usafirishaji, pamoja na shughuli za forodha baina ya Russia na Iran, ni miongoni mwa maeneo ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi mbili; na maafisa wa pande husika wanaendelea kufuatilia utekelezaji wake katika mikutano mbalimbali.

Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Russia amekubali pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kupanuliwa zaidi uhusiano wa kiuchumi na kusema: “Uhusiano wa Iran na Russia ni wa kina na wa kimkakati. Mwaka jana pekee (2021), mabadilishano ya kifedha kati ya nchi hizi mbili yaliongezeka kwa asilimia 81, na katika miezi ya kwanza ya mwaka huu yamekuwa kwa asilimia 31; hali hii ni ya kuridhisha na ina maslahi kwa nchi zote mbili.”

Mazungumzo ya Rais Ebrahim Raisi na Putin

Ni wazi kuwa, kupatikana mbinu na njia zinazohitajika za kuimarisha uhusiano wa kibenki na kifedha kati ya Iran na Russia ambazo hazitaathiriwa na ushawishi na mashinikizo ya Magharibi na kufanya kazi kwa uhuru na kujitegemea, kutaimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na kutayarisha mazingira mazuri ya ushirikiano zaidi.

Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali anasema: Maafisa wa masuala ya uchumi na benki wa Iran na Russia wamekuwa kwenye mawasiliano ya mara kwa mara kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja hizo, na inaonekana kuwa, katika siku chache zijazo tutashuhudia mkutano wa maafisa wa nchi hizi mbili utakaojadili masuala ya kuondoa baadhi ya visingiti vilivyopo katika sekta hii.