Jul 02, 2022 11:49 UTC
  • Mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Tanzania yameongezeka kwa 120%

Balozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania amesema, mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili katika mwaka uliopita yaliongezeka kwa asilimia 120.

Hossein Alvandi ameyasema hayo katika kikao cha wawakilishi wa vyama vya wafanyabiashara wa Iran na Tanzania kilichofanyika kwa njia ya intaneti na akaongezea kwa kusema, kuna fursa na mazingira mazuri pia ya ushirikiano katika nyanja za tiba na teknolojia ya taaluma.

Katika kikao hicho, rais wa chama cha wafanyabiashara, viwanda na wakulima Tanzania (TCCIA) Paul Koyi amesema, sekta za nishati, petrokemikali, madini na kilimo ni miongoni mwa nyanja muhimu zaidi za ushirikiano baina ya wadau wa kiuchumi wa nchi mbili na akataka mashirika ya Kiirani yashiriki kwa wingi zaidi katika miradi ya kiuchumi nchini Tanzania.

Paul Koyi

Shahram Khasipour, mkurugenzi wa chama cha wafanyabiashara Iran kwa nchi za Kiarabu na Kiafrika yeye ameashiria umuhimu wa Tanzania kama daraja la kuiunganisha Iran na ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa pia na uthabiti wa kisiasa unaozidi kuongezeka pamoja na miundomsingi ya uchukuzi na usafirishaji wa baharini katika bandari ya Dar es Salaam; na akasema: jambo hili pamoja na nafasi ya kistratejia na uwezo ilionao Iran vinalifanya suala la kustawisha uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili liwe na umuhimu maalumu.

Washiriki wa kikao hicho wamejadili pia kukosekana safari za moja kwa moja za ndege kati ya nchi mbili, miundomsingi ya usafirishaji, mabadilishano ya kifedha na kibenki, utekelezaji wa makubaliano, matatizo ya forodha na vizuizi vinavyokwamisha kustawishwa uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Tanzania.../

 

Tags