Jul 02, 2022 12:27 UTC
  • Iran: Tunapinga hatua yoyote ya kijeshi inayochukuliwa kwa kisingizio chochote kile

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "sisi tunauelewa wasiwasi ilionao nchi jirani yetu Uturuki na tunapinga vikali hatua yoyote ya kijeshi inayochukuliwa kwa kisingizio chochote kile".

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Damascus nchini Syria.

Baada ya ziara aliyofanya siku chache zilizopita nchini Uturuki, Amir-Abdollahian leo alielekea Syria.

Katika safari yake ya saa kadhaa mjini Ankara, waziri wa mambo ya nje wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na waziri mwenzake pamoja na rais wa Uturuki juu ya matukio ya eneo yakiwemo ya nchini Syria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Damascus, Amir-Abdollahian amesema, Iran inalaani vikali uchokozi uliofanywa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya umoja wa ardhi ya Syria na akaongezea kwa kusema: mbali na vikwazo vinavyotekelezwa dhidi ya wananchi wanamuqawama wa Syria, wazayuni wanalenga kuvuruga uthabiti nchini humo na kuwaongezea matatizo na masaibu mengine wananchi hao.

Hossein Amir-Abdollahian (kati) akiwa na Faisal Miqdad (kushoto)

Waziri wa mambo ya nje wa Iran amebainisha kuwa, wananchi, serikali na uongozi wa Syria wamesimama imara kulinda umoja wa ardhi yao kwa nguvu na uwezo wao wote na akaongezea kwa kusema: "sisi tunauelewa wasiwasi ilionao nchi jirani yetu Uturuki na tunapinga vikali hatua yoyote ya kijeshi inayochukuliwa kwa kisingizio chochote kile; na tunafanya juhudi kupitia njia za kidiplomasia na mazungumzo ya kisiasa ili kutatua sutafahamu  zilizopo baina ya Syria na Uturuki".

Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal al Miqdad amewaeleza waandishi wa habari pembeni ya hafla ya kumlaki waziri mwenzake wa Iran kuwa, Syria inafuatlia kwa uzito kamili faili la nyuklia la Iran na kwamba iko pamoja na Jamhuri ya Kiislamu na inaunga mkono msimamo wa Tehran katika kadhia hiyo.../

Tags