Jul 03, 2022 04:19 UTC
  • Gharibabadi: Nchi zilizohusika na jinai ya mabomu ya kemikali Sardasht ziwajibishwe

Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria jinai za Marekani katika kuunga mkono utawala ulioangushwa wa Saddam wakati wa vita vyake vya kulazimishwa dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa: "Nchi zote zilizohusika kwa njia moja au nyingine katika udondoshaji mabomu huko Sardasht zinapaswa kuwajibishwa."

Tarehe 28 Juni, 1987 utawala wa Saddam wa chama cha Baath nchini Iraq ulitumia mabomu ya kemikali kushambulia maeneo manne ya mji wa Sardasht  nchini Iran yaliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu. Katika shambulio hilo la kinyama, raia  110 wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 8,000 waliathirika kwa gesi ya sumu ya silaha hizo.

Akizungumza kwa mnasaba wa tukio hilo chungu ambalo nchini Iran hukumbukwa sambamba na 'Wiki ya Kufichuliwa Utambulisho Halisi wa Haki za Binadamu za Kimarekani', Kazem Gharibabadi Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Magharibi zilihusika katika vitendo vya kigaidi vya utawala wa Saddam wakati  utawala huo ulipodondosha mabomu ya kemikali mjini Sardasht.

Gharibabadi amesema nchi za Magharibi zilihusika katika jinai hiyo ya Sardasht na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muhanga wa silaha za maangamizi ya umati. Kutokana na utumizi wa silaha za kemikali, karibu Wairani 13,000 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya laki moja walijeruhiwa. Aidha waliopata majeruhi kutokana na silaha za kemikali hufa shahidi kila siku nchini Iran."

Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran anasema, kwa mujibu wa ripoti za miaka ya hivi karibuni za Shirika la Kimataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Nyuklia lenye makao yake The Hague, zaidi ya nchi 15, aghalabu zikiwa ni za Ulaya na Marekani zilihusika katika kumpa Saddam silaha za kemikali na kwa msingi huo zinapaswa kuwajibishwa kisheria.

Gharibabadi ameendelea kusema kuwa mashirika ya kimataifa na ya kutetea haki za binadamu yanapaswa kuziwajibisha nchi husika. Ameongeza kuwa, kumefikishwa mashtaka dhidi ya raia bainafsi wa Ulaya waliohusika lakini hilo halitoshi. 

Utumiaji wa silaha za kemikali umepigwa marufuku kulingana na mikataba na makubaliano ya kimataifa. 

Ripoti mbalimbali zinaonyesha pia kuwa, kuna mashirika zaidi ya 400 yanayozalisha mada za kemikali, ambapo mengi ni ya Ujerumani na Uingereza, ambayo yalichangia katika kuuzatiti utawala wa Baath wa Iraq kwa silaha za kemikali.