Jul 03, 2022 04:34 UTC
  • Abdollahian: Palestina ndio kadhia muhimu zaidi kwa umma wa Kiislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ukombozi wa taifa la Palestina ndio kadhia muhimu zaidi kwa umma wa Kiislamu hivi sasa.

Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana huko Damascus, mji mkuu wa Syria katika kikao na makundi ya Wapalestina yaliyoko nchini Syria na kueleza kuwa, taifa la Iran litaendelea kuunga mkono muqawama na mapambano ya Wapalestina, mpaka pale watakapopata ushindi wa kuikomboa ardhi yao, mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu.

Amir-Abdollahian ameashiria haja ya kuwepo msimamo wa pamoja baina ya nchi za Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina na kueleza bayana kuwa, Iran inalaani vikali uchokozi unaofanywa mara kwa mara na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya umoja wa ardhi ya Syria.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameashiria operesheni za kijeshi za Uturuki nchini Syria na kubainisha kuwa, operesheni hizo hazitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kusababisha ukosefu wa uthabiti katika eneo zima la Asia Magharibi. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kadhalika jana Jumamosi alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Bashar al-Assad wa Syria, ambapo amezikosoa nchi za Magharibi kwa undumakuwili wao, na kutoa madai hewa yasiyo na uhalisia juu ya mustakabali wa Syria.

Rais Bashar al-Assad wa Syria (kulia) na Hossein Amir-Abdollahian mjini Damascus

Amesema: Kushindwa kukabiliana na hatua haribifu za utawala wa Kizayuni, kunaonesha kuwa madai ya nchi za Magharibi kuwa zinafanya jitihada za kuirejeshea Syria uthabiti hayana ukweli wowote.

Kwa upande wake, Rais Bashar al-Assad wa Syria mbali na kusisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa zaidi ya miaka 40 wa pande mbili wa Tehran na Damascus katika nyuga tofauti, amepongeza uungaji mkono na juhudi za Iran za kutaka kuliondoa taifa la Syria kwenye kinamasi cha vita.

Tags