Jul 04, 2022 14:10 UTC
  • Raisi: Historia haitasahau kamwe uhalifu wa Marekani dhidi ya taifa la Vietnam

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika hafla ya kupokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Vietnam mjini Tehran kwamba historia haitasahau kamwe jinai zilizofanywa na Marekani dhidi ya taifa la Vietnam.

Inakadiriwa kuwa, zaidi ya watu milioni tatu waliuawa wakati wa vita vya Marekani dhidi ya taifa la Vietnam. 

Vilevile karibu galoni milioni 18 na laki mbili sumu zilirushwa na ndege za kivita za Marekani kwa watu wa Vietnam tangu mwaka 1961 hadi 1971, na serikali ya Vietnam ilitangaza kuwa watu 400,000 waliuawa na sumu hiyo ya kemikali, na watoto laki tano (500,000) wamezaliwa wakiwa na kasoro za viungo na ulemavu.

Akizungumza na balozi mpya wa Vietnam mjini Tehran, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, amesema kwamba Iran inawatambua Wavietnamu kuwa ni watu waliosimama kidete kupinga ukoloni na utawala wa kimabavu, na kwamba nchi mbili za Iran na Vietnam zina misimamo inayofanana katika uwanja huo.

Raisi pia ameashiria uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Tehran na Hanoi na kueleza kuwa, kiwango cha hivi sasa cha ushirikiano na uhusiano kati ya Iran na Vietnam hakilingani na uwezo wa nchi hizo mbili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kilimo, teknolojia na uchukuzi.

Kwa upande wake Long Kok Hui, balozi mpya wa Vietnam nchini Iran amesema kwamba Wairani ni wapenda amani na watu wenye utamaduni na ustaarabu tajiri na wa kihistoria. Ameongeza kuwa, licha ya vikwazo na mashinikizo ya miaka mingi, Iran imepata maendeleo na mafanikio makubwa. 

Kok Hui amesema Vietnam daima imekuwa na uhusiano mzuri na Iran na inajitahidi kuboresha kiwango cha ushirikiano hususan katika nyanja za uchumi na biashara.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Vietnam iliunga mkono mapinduzi ya wananchi wa Iran, na marais watatu wa Jamhuri ya Kiislamu ambao ni Hassan Rouhani mwaka 2016, Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2012 na Akbar Hashemi Rafsanjani mwaka 1995 walitembelea nchi ya Vietnam.