Jul 05, 2022 03:07 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mazungumzo yenye tija yanahitaji Marekani kuwa na nia ya dhati na kuwa tayari kubadilika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, mazungumzo yenye tija yanategemea upande wa Marekani utakavyokuwa na nia ya dhati, ubunifu na kuwa tayari kubadilika.

Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya Jumatatu kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Sayyid Badr Albusaidi ambapo sambamba na sisitizo hilo amebainisha kuwa, Iran ina nia ya dhati ya kufikia makubaliano imara na endelevu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ametilia mkazo mtazamo wa nchi yake kuhusu umuhimu wa kufikiwa mwafaka na makubaliano rasmi katika mazungumzo na akasema: Oman siku zote imekuwa ikiunga mkono kufikiwa mwafaka katika mazungumzo ya nyuklia; na Iran kutimiziwa matakwa yake halali na ya kisheria.

Katika mazungumzo hayo ya simu wanadiplomasi hao wakuu wa Iran na Oman wamebadilishana mawazo pia kuhusu baadhi ya masuala yanayopewa umuhimu wa pamoja katika nyuga za pande mbili, kikanda na kimataifa, ikiwemo hali ya mazungumzo ya kuiondolea vikwazo vya kidhalimu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mbali na mazungumzo hayo ya simu aliyofanya na mwenzake wa Oman hapo jana, siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alizungumza kwa njia ya simu pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna na kumweleza kwamba, tathmini ya Iran ni ya mtazamo chanya kuhusiana na mazungumzo ya karibuni yaliyofanyika Doha, Qatar, lakini inapasa kuona ni vipi upande wa Marekani unataka kuitumia fursa iliyopo ya diplomasia.

Amir-Abdollahian ameeleza kuwa katika mazungumzo, Iran imekuwa kila mara ikiwasilisha mapendekezo na rai chanya na akaongezea kwa kusema, sasa hivi njia ya diplomasia iko wazi na Iran ni mkweli na ina nia ya dhati ya kufikia hatua ya mwisho ya mwafaka ulio mzuri na endelevu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikiheshimu ahadi na kutekeleza majukumu yake na inavyotarajia, pande zote katika upande wa pili, nazo pie zitekeleze kwa usahihi ahadi na majukumu yao.../