Jul 06, 2022 13:34 UTC
  • Rais wa Iran: Kuimarisha mabadilishano ya kibiashara na nchi za eneo ni dharura

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuna udharura wa kutumia fursa zilizojitokeza kuimarisha uhususiano wa kibiashara na nchi za eneo.

Rais Ebrahim Raeisi ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa kuna udharura wa kuimarisha mabadilishano ya kibiashara na nchi za eneo hasa nchi jirani.

Aidha ametoa wito wa kutumiwa fursa iliyojitokeza ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa ndani ya nchi ili kuimarisha sekta ya viwanda na kutekeleza miradi ya pamoja na nchi za eneo hasa utekelezwaji wa mradi wa uchukuzi wa Korido ya Rasht-Astara na kuendelezwa hadi  Jamhuri ya Azerbaijan.

Kikao cha Baraza la Mawaziri Iran

Hali kadhalika ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje kuchukua hatua za kuhakikisha mapatano yaliyotiwa saini baina ya Iran na nchi zingine yanatekelezwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hali kadhalika ameashiria kutiwa saini mapatano yenye thamani ya dola bilioni saba kwa ajili ya kustawisha visima vya mafuta vya pamoja katika eneo la Azadegan na kusema hatua hii ni mfano wa wazi wa kutegemea uwezo wa ndani ya nchi katika utekeleza miradi muhimu ya uzalishaji. Amesema  ushiriki wa benki katika utekelezaji wa miradi kama hiyo ni jambo ambalo litapelekea sekta binafsi iwekeze zaidi ndani ya nchi.