Jul 07, 2022 08:20 UTC
  • Shamkhani: Tumeingia katika mazungumzo ya kuondoa vikwazo ili kufikia makubaliano imara, endelevu na ya kuaminika

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar hapa Tehran kuwa Iran imeingia katika mazungumzo ya kuondoa vikwazo ili kufikia makubaliano imara, endelevu na ya kuaminika.

Sheikh Muhammad bin Abdulrahman Al Thani Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye amefanya ziara hapa nchini amekutana na kuzungumza na Admeri Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na kutupia jicho masuala mbalimbali ya pande mbili, kikanda na matukio ya kisiasia na kiusalama ya karibuni katika eneo. 

Katika mazungumzo hayo, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameeleza kuwa, sera za siku zote za Iran mkabala wa majirani zake ni kustawisha uhusiano wa pande zote, wa kimkakati na ujirani mwema. 

Ali Shamkhani ameongeza kuwa ugaidi na Uzayuni ni mambo mawili makuu yanayosababisha machafuko katika eneo na kwamba hatua yoyote ya kuungana na utawala wa Kizayuni  ni tishio kwa amani na usalama wa eneo. "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikidhihirisha hamu yake katika usalama wa pamoja na kulindwa umoja wa ardhi za nchi za eneo kama stratejia yake ya siku zote" amesema Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran". 

Wakati huo huo, Ali Shamkhani amebainisha kuwa, vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran vinapasa kuondolewa  ili nchi zote ziweze kuwekeza kwa urahisi hapa nchini kwa kulindwa maslahi ya muda mrefu. 

Katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameeleza kufurahishwa na ziara yake mjini Tehran na kusisitiza juu ya udharura wa kuendelezwa mazungumzo ya kikanda ili kuondoa baadhi ya vizuizi bandia vilivyopo na kuharakisha ustawi wa mahusiano ya pande mbili na pande kadhaa kati ya nchi mbalimbali za eneo. 

Ali Shamkhani katika mazungumzo na Muhammad Abdulrahman al Thani mjini Tehran

 

Tags