Jul 07, 2022 10:52 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar nchini Iran wiki moja baada ya mazungumzo ya Doha

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Jumatano alifika mjini Tehran na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amekutana na Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambapo mbali na kuzungumza kuhusu uhusiano wa pande mbili wamebadilishana mawazo kuhusu masuala yenye umuhimu kwa pande mbili katika uga wa kieneo na kimataifa.

Qatar inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopewa kipaumbele katika siasa za nje za Iran. Nchi hizi mbili za Kiislamu ziko katika eneo muhimu na nyeti la Ghuba ya Uajemi, na misimamo yao katika masuala muhimu ya eneo inakaribiana. Katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kuwekewa vikwazo Qatar na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri na jibu chanya la Iran la kuwasaidia wananchi na serikali ya Qatar katika kuvunja vikwazo hivyo, uhusiano wa kisiasa wa nchi hizo mbili ulifikia viwango vya juu zaidi.

Rais wa Iran Seyed Ebrahim Raisi alikwenda Qatar katika safari yake ya nne ya nje ya nchi tarehe 21 Februari, safari ambayo ilikaribishwa vyema na Amir wa Qatar na, kwa mujibu wa wataalamu na wachambuzi, safari hiyo ilikuwa na mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kiusalama.

 Katika safari hiyo ya rais wa Iran nchini Qatar, mikataba 14 ya makubaliano ilisainiwa katika nyanja za safari za ndege, meli, biashara, vyombo vya habari, kufuta visa, umeme, elimu na utamaduni baina ya pande hizo mbili, na baada ya hapo, mamlaka za nchi hizo mbili zilishauriana na lengo la kupanua ushirikiano katika masuala ya nchi mbili na kikanda na kimataifa kuongezeka.

Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar mjini Tehran siku ya Jumatano pia inafanyika baad ya Doha kuwa mwenyeji wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kwa upatanishi wa Umoja wa Ulaya wiki iliyopita (Juni 28 na 29).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameutaja mchakato wa mazungumzo hayo kuwa chanya na akiashiria vikao vyake tofauti na wajumbe wa mazungumzo hayo, amesema: Wakati ikizingatiwa awamu hii ya mazungumzo ilikuwa muhimu, Qatar iko kwenye njia ya kuendelea kuandaa mazungumzo hadi kufikiwa matokeo yanayotarajiwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na itafanya juu chini kuhakikisha pande zote zinarejea katika utekelezaji wa ahadi zao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar (kushoto) na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran

Wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo ulazima wa kuzingatiwa uhalisia na kuchukuliwa maamuzi ya kisiasa huko Washington ili kufikia makubaliano mazuri, yenye nguvu na thabiti, na imewasilisha mipango muhimu kwa ajili hiyo, maafisa wa Marekani wanadai kuwa Iran katika mazungumzo ya Doha iliibua matakwa "yaliyo nje ya JCPOA" ambayo ni ishara ya kuwa Tehran halipi suala hilo uzito na kuwa haina dhamira ya kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Katika hali hiyo, Ned Price, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema Jumanne kwamba Washington hivi sasa haina mpango wa kufanya duru nyingine ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran.

Pamoja na hayo, maneno ya "Sheikh Mohammad bin Abdulrahman Al-Thani" kuhusu juhudi za nchi yake za kuendelea kuandaa mazungumzo kwa lengo la kufuta vikwazo dhidi ya Iran, yanaimarisha uwezekano wa suala hili kuwa moja ya mihimili mikuu ya mashauriano yake mjini Tehran. Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar pia amekutana na "Ali Shamkhani", katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.