Jul 21, 2022 07:34 UTC
  • Rais wa Iran apongeza mapambano ya watu wa Syria

Rais Ebrahim Raeisi wa Iran amesema ana yakini kuwa Syria ina mustakakbali mwema huku akiwapongeza wananchi wa Syria kwa mapambano na muqawama katika kipindi cha miaka 11 ya vita dhidi ya nchi hiyo ambavyo vinaungwa mkono na madola ya kigeni.

Raisi aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al Mikdad aliye safarini mjini Tehran. Raisi ameunga mkono kauli ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambaye amesema Marekani haina budi ila kuondoka nchini Syria. Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kuondoka askari vamizi wa Marekani mashariki mwa Mto Furati na eneo lote ni suluhisho la kimsingi kwa migogoro ya Asia Magharibi.

Aidha Raisi amesisitiza kuhusu haja ya jeshi la Syria kuchukua udhibiti kamili wa mipaka yote ya nchi hiyo.

Kwa upande wake, Mikdad amewasilisha salamu za Rais Bashar al Asad wa Syria kwa viongozi wa Iran. Aidha ameipongeza Iran kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Jumanne wa viongozi wa Iran, Russia na Uturuki ambao uliitishwa kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mgogoro wa Syria.

Marais wa Russia, Iran na Uturuki wakielekea katika mkutano kuhusu kadhia ya Syria mjini Tehran

Amesema kauli za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais wa Iran ni ishara ya muungano wa Tehran na Damascus.

Mapema Jumatano pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Feisal Miqdad walishiriki katika kikao cha pamoja na waandishi habari na kusisitiza kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Syria.

Tags