Jul 21, 2022 12:09 UTC

Afisa wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za kimuqawama zinapaswa kuendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano wao ili zifanikiwe kuwatimua wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Syria na katika eneo lote la Asia Magharibi.

Ali Akbar Velayati, Mshauri mkuu wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal al Mikdad.

Velayati ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi wa Syria bila uoga wowote.

Amesema, "Syria ni mwanachama muhimu wa mrengo wa muqawama na Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikiunga mkono na itaendelea kuunga mkono kambi ya mapambano."

Dakta Velayati amebainisha kuwa, Iran imezuia kugawanywa nchi ya Syria kama ilivyofanyika huko Libya na wakati huo huo inaisadia serikali halali ya Damascus kukabiliana na chokochoko za Marekani. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Syria mjini Tehran

Hali kadhalika Ali Akbar Velayati, Mshauri mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema utawala wa Kizayuni na vibaraka wake ni dhaifu mno na hawawezi kuiteteresha kambi ya muqawama.

Aidha ameipongeza Syria kwa kutofuata mkumbo wa baadhi ya madola katika eneo hili wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

 

Tags