Jul 24, 2022 07:34 UTC
  • Mazungumzo kati ya marais wa Iran na Ufaransa; Raisi akosoa sera za kuzusha migogoro za Wamagharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, zzimio lililotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki dhidi ya Iran ni hatua ya kuzusha mgogoro iliyokuwa na lengo la kuliwekea mashinikizo taifa la Iran.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Amekosoa hatua na misimamo hasi ya Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Iran na kusema: Azimio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) lilikuwa na taathira hasi kwa hali ya kuaminiana ya kisiasa.

Azimio hilo lililopendekezwa na Marekani pamoja na Troika ya Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, lilipasishwa mwezi uliopita wa Juni na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia. Kuidhinishwa kwa azimio hilo ambalo lilitokana na ripoti isiyo na mizani ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo na kwa msingi wa habari za uongo na uzushi za utawala wa Kizayuni wa Israel, kulikabiliwa jibu la Iran. Baada tu ya hatua hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa jibu mwafaka kwa hatua za kivitendo ikiwa ni pamoja na kusimika mashinepewa za kisasa (centrifuges) na kuzima kamera za wakala wa IAEA katika baadhi ya taasisi zake za kuzalisha nishati ya nyukia. 

Hatua hiyo dhidi ya Iran ya Marekani na Troika ya Ulaya ilionyesha kuwa pande za Magharibi katika mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran zinatumia azimio la kisiasa la wakala wa IAEA kama chombo cha kuishinikiza Iran na kufidia mkwamo wao katika mazungumzo ya Vienna.

IAEA

Kwa maneno mengine ni kwamba, Marekani ilijaribu kuongeza uwezo wake wa kujadiliana katika mazungumzo ya nyuklia na Iran kwa kutumia vibaya wakala wa IAEA na masuala ya kiufundi ili kuilazimisha Iran irudi nyuma na kulegeza kamba katika matakwa yake ya kisheria na halali.

Ni wazi kuwa, kuendelezwa vikwazo dhidi ya Iran, kutolewa azimio katika wakala huo na kutumia sera za kindumakuwili na mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya Iran hakuwezi kujenga imani, bali ni dhihirisho la sera za ubabe na kupenda makuu za serikali ya Washingon na washirika wake. Hii ni licha ya kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara kwa mara kwamba kamwe haitasalimu amri mbele ya sera na siasa hizo za kibeberu.

Katika mazungumzo yake na Emmanuel Macron, Rais Ebrahim Raisi amesema anaitakidi kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa iwapo masuala yenye utata yatapatiwa ufumbuzi, sanjari na kutoa dhamana upande wa pili wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kudhaminiwa maslahi ya kiuchumi ya taifa la Iran.

Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria ukuaji mkubwa wa ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa Iran na nchi mbalimbali za dunia na kuvitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kuwa vina madhara kwa uchumi wa dunia hususan Ulaya.

Baada ya kuwekwa vikwazo vya nchi za Magharibi katika sekta ya nishati ya baadhi ya nchi zikiwemo Iran na Russia, bei ya mafuta na petroli katika nchi za Magharibi hasa za Ulaya ambazo zinategemea sana uagizaji wa nishati hiyo kutoka nje, imeongezeka kwa kiasi kikubwa na nchi hizo zimekabiliwa na matatizo katika kudhamini nishati. Suala hili limeilazimisha hata Ufaransa kutoa wito wa kurejeshwa kwa mafuta ya Iran na Venezuela katika masoko ya kimataifa ili kuzuia ongezeko la bei ya bidhaa hiyo.

Kuhusiana na suala hilo, shirika la habari la Bloomberg limeashiria panda shuka zinazoshuhudiwa katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA kwa ajili ya kundoa vikwazo dhidi ya Iran na kuandika kuwa: "Matumaini ya Rais Joe Biden wa Marekani ya kuyafufua mapatano hayo yanafifia, licha ya kwamba dunia inahitaji mafuta zaidi kuliko hapo awali."

Joe Biden

Kwa hiyo, msukosuko wa soko la nishati duniani utahatarisha usalama wa nishati na kutayarisha mazingira yanayowatia wasiwasi waagizaji wa mafuta wa Ulaya, hasa katika majira ya baridi. Hapana shaka yoyote kwamba, miongoni mwa sababu kuu za mazingira hayo ni vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi hususan Marekani dhidi ya Iran, nchi ambayo ni miongoni mwa mataifa yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani.

Tags