Jul 29, 2022 10:50 UTC
  • Ayatullah Khatami: Wanawake Wairani wameweza kunawiri katika sekta zote wakiwa na Hijabu ya Kiislamu

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran amesema kuwa, wanawake Wairani wameweza kunawiri katika sekta za kielimu, kisiasa, kiuchumi na usimamizi huku wakiwa wanazingatia Hijabu, vazi la staha la Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami, Khatibu na Imamu wa Muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria kadhia ya hijabu na kujisitiri na kusema madola ya Magharibi yamekuwa yakipiga vita Hijabu.  Ameendelea kusema kuwa maadui wanakasirishwa na vazi la Hijabu la mwanamke Mwislamu na hivyo wanatekeleza njama za kuibua shubha kuhusu vazi hilo.

Kwingineko katika hotuba yake, Ayatullah Khatami amesema madola ya kibeberu na kiistikbari duniani yakiongozwa na Marekani yanapinga Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW.

Ameendelea kusema kuwa, madola hayo ya kibeberu hayapendezwi hata kidogo na Uislamu ulioko katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hata hivyo amesema, “Ulimwengu wa kiistikbari utake usitake, hautaweza kuiondoa Iran ya Kiislamu katika njia ya Uislamu, Qur’ani na Ahul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.” Amesisitiza kuwa, taifa la Iran daima litaendelea kusimamia Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW.

Wanawake nchini Iran wakiwa wamevalia Hijabu

Kwingineko katika hotuba yake, Ayatullah Khatami ameashiria mkutano wa hivi karibuni wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Marais Vladimir Putin wa Russia na Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki na kusema: “Kiongozi Muadhamu katika mkutano na Erdogan alisisitiza kuwa kuna umuhimu katika kulinda mipaka na mamlaka ya kujitawala Syria kikamilifu. Msimamo huo wa kiongozi Muadhamu ulikuwa ni wenye busara.”

Aidha amesema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemfahamisha Rais Putin wa Russia kuwa anasikitishwa na mauaji ya watu wa kawaid katika vita vya Ukraine lakini wakati huo huo akasema iwapo Russia haingechukua hatua ya kwanza katika kadhia ya Ukriane, basi upande wa pili ungeanzisha uhasama.

Ayatullah Khatami ameashiria kuwadia Mwezi wa Muharram ambamo Waislamu huomboleza kuuawa shahidi Imam Hussein AS na kusema:"Kumi la kwanza la Muharram ni kumi la kuhuisha amri ya kuamurisha mema na kukataza mabaya na kuongeza kuwa: "Kuimarisha mfumo wa Kiislamu ni jambo jema zaidi na kuudhoofisha mfumo wa Kiislamu ni jambo baya zaidi."

 

 

Tags