Aug 03, 2022 12:32 UTC
  • Mjukuu wa Mandela: Mapinduzi ya Kiislamu yameipa ilhamu Afrika Kusini

Mjukuu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanatoa ilhamu na motisha kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Mandla Mandela ambaye yuko hapa Tehran kwa ajili ya kupokea Tuzo ya Haki za Binadamu za Kiislamu amesema hayo katika mazungumzo yake na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kueleza kuwa, mbali na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulipa ilhamu taifa hilo la kusini mwa Afrika, lakini yalimpa nguvu na msukumo hayati Nelson Mandela, alipofungwa jela katika enzi za utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid).

Amekumbusha kuwa, katika Mkutano Mkuu wa 52 wa chama tawala cha ANC, wajumbe wote kwa kauli moja walitoa mwito wa kupunguzwa uhusiano wa Afrika Kusini na Israel. 

Aidha amesema nchi hiyo, Algeria pamoja na nchi nyingine za Afrika zilipinga azma ya kuujumuisha utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwa mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Afrika (AU). 

Mbali na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Iran na Afrika Kusini, mjukuu huyo wa Mandela ambaye alikuwa shujaa wa kupambana na mfumo wa ubaguzi wa apartheid amesisitiza kuwa, hatua ya makundi na harakati za Palestina ya kusimama kidete dhidi ya Israel ambayo ni nembo ya apartheid, ina umuhimu mkubwa.

Mzee Mandela na mjukuu wake Mandla

Kwa upande wake, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemshukuru Mandla Mandela kwa jitihada zake za kuimarisha uhusiano wa Afrika Kusini na Iran, na vile vile kwa uungaji mkono wake usio na kikomo kwa taifa la Palestina.

Kadhalika amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapongeza misimamo ya hayati Nelson Mandela na chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ya kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina.

Tags