Aug 04, 2022 11:22 UTC
  • Ujumbe wa Iran wawasili Vienna, mazungumzo ya uondoaji vikwazo yaanza

Ujumbe wa Iran umewasili mjini Vienna kwa ajili ya duru mpya ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambayo imepangwa kuanza leo.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukiongozwa na mkuu wa timu ya mazungumzo Ali Baqeri Kani uliwasili katika mji mkuu wa Austria Vienna leo asubuhi kwa lengo la kushiriki katika duru mpya ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu vya Marekani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, mazungumzo kati ya ujumbe wa Iran na pande zingine husika katika mazungumzo hayo yalitazamiwa kuanza hii leo pia.

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Twitter hapo jana kabla ya kuelekea Vienna, Ali Baqeri Kani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema: "Ninaelekea Vienna kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo; wanaobeba dhima ni wale waliokiuka makubaliano na kushindwa kuachana na mirathi ya nuhusi ya huko nyuma."

Mjumbe huyo mwandamizi wa timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongezea kwa kusema: Marekani inapaswa ishukuru na kuthamini fursa iliyoandaliwa kwa ukarimu wa wanachama wa JCPOA; mpira uko kwenye uwanja wao ili waonyeshe ukomavu na kuchukua hatua kiuwajibikaji.

Mapema jana Jumatano, katika mazungumzo aliyofanya mjini Tehran na Pasquale Ferrara, Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Nje na Usalama wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Baqeri Kani alisema, Marekani haiwezi kuiwekea masharti Iran ambayo ni mwanachama wa JCPOA na akaongeza kwamba, katika mazungumzo yajayo itapimwa na kutathminiwa Marekani kama ina irada na azma ya dhati ya kufikia mwafaka na makubaliano.

Mapema wakati akitangaza safari ya ujumbe wa Iran kuelekea Vienna, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Nasser Kanaani Chafi alisema: katika duru hii ya mazungumzo, pande husika zitabadilishana mawazo kuhusu rai mpya za kila upande zikiwemo zilizopendekezwa na Iran.../