Aug 06, 2022 03:53 UTC
  • Iran: Kinachotugusa zaidi katika mazungumzo ya nyuklia ni manufaa kiuchumi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kinachoishughulisha zaidi Tehran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna ni manufaa yake ya kiuchumi.

Hossein Amir-Abdolahian amesema hayo wakati alipokuwa anawasilisha ripoti yake katika Kamati ya Kifungu cha 90 cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kuhusu mchakato wa mazungumzo ya Vienna ya kuondolewa Tehran vikwazo.

Ameongeza kuwa, lililo muhimu zaidi kwa timu ya mazungumzo ya Iran, ni manufaa ya kiuchumi ya taifa hili, kuchunga mistari myekundu na kulindwa uwezo wa kielimu na kiteknolojia wa ndani ya Iran wa kunufaika kwa njia ya amani na nishati ya atomiki.

Juzi Alkhamisi, ujumbe wa Iran uliwasili mjini Vienna Austria kwa ajili ya kushiriki katika awamu mpya ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu vya Marekani. Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliongozwa na mkuu wa timu ya mazungumzo Ali Baqeri Kani na uliwasili katika mji mkuu wa Austria Vienna Alkhamisi asubuhi.

Ali Bagheri Kani, mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna

 

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Twitter siku ya Jumatano kabla ya kuelekea Vienna, Ali Bagheri Kani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa alisema: "Ninaelekea Vienna kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo; wanaobeba dhima ni wale waliokiuka makubaliano na kushindwa kuachana na mirathi ya nuhusi ya huko nyuma."

Mapema siku hiyo hiyo ya Jumatano na katika mazungumzo aliyofanya hapa Tehran na Pasquale Ferrara, Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Nje na Usalama wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Baqeri Kani alisema, Marekani haiwezi kuiwekea masharti Iran ambayo ni mwanachama wa JCPOA na akaongeza kwamba, katika mazungumzo yajayo itapimwa na kutathminiwa Marekani kama ina nia na azma ya dhati ya kufikia mwafaka na makubaliano au la.

Tags