Aug 06, 2022 11:00 UTC
  • Raisi alaani ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina Gaza, IRGC yatoa neno

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyopelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa makumi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo Jumamosi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Katika jinai zake za jana usiku, utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine umeionesha dunia dhati yake halisi ya ukatili na kukalia kwa mabavu ardhi (za Wapalestina)."

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, muqawama na mapambano ya watu wa Ukanda wa Gaza yatakuwa chachu ya kuporomoko na kusambaratika kwa utawala huo unaoua watoto wa Palestina.

Jana alasiri, ndege za kivita za utawala haramu wa Israel ziliushambulia Ukanda wa Gaza na  kuua watu 15 akiwemo kamanda mwandamizi wa Harakati ya Jihad Islami,Taysir al Jabari na mtoto wa miaka mitano mjini Rafah, kusini mwa eneo hilo ambalo liko chini ya mzingiro wa Israel.

Wakati huohuo, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema utawala ghasibu wa Israel upo katika ncha ya kuporomoka.

Bigedia Jenerali Esmail Ghaani

Bigedia Jenerali Esmail Ghaani amesema hayo katika hafla ya kumbukumbu ya mashahidi wa Haram Tukufu na kubainisha kuwa, operesheni 15 zinafanyika kila siku dhidi ya maeneo ya utawala huo pandikizi. Amesema vikosi vya SEPAH vinafuatilia kwa jicho la karibu nyendo haribifu za utawala wa Kizayuni na Marekani.

Kabla ya hapo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani pia hujuma ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kusema: "Palestina ina haki ya kisheria ya kujilinda mbele ya hatua za kigaidi za Israel."

Ukatili wa Israel katika Ukanda wa Gaza

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imevurumisha makombora zaidi ya 100 katika ardhi zilizopachikwa jina la Israel ikiwa ni katika kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya utawala huo katili ya kumwaga damu za Wapalestina Gaza.

 

Tags