Aug 08, 2022 03:10 UTC
  • Ushujaa wa vijana wa Palestina, Yemen ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani jinai zinazofanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza, amesema ushujaa wa vijana wa Palestina na Yemen ni muendelezo wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana usiku katika marasimu ya usiku wa mwezi kumi Mfunguo Nne, Muharram, wa kuamkia Ashura ya Imam Hussein AS.

Sayyid Raisi amebainisha kuwa, ushujaa uliooneshwa na kambi ya muqawama huko Palestina ni matunda ya moyo wa kusimama kidete dhidi ya ubeberu na kujiamini uliozalishwa na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Ameeleza bayana kwamba, kuwa macho na kusimama kidete vijana wa eneo hili la Asia Magharibi kumetokana na damu ya Mashahidi.

Rais Raisi katika kikao cha kumuomboleza Imam Hussein AS

Rais wa Iran amebainisha kuwa, Wazayuni katika hujuma zao za kigaidi wamewashambulia wakazi wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza, na kwamba Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imewashambulia Wazayuni kujibu uchokozi na ukatili wa utawala huo haramu.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesisitiza kuwa, "Hii leo wananchi wa Palestina si kama walivyokuwa huko nyuma, kufungamanisha matumaini yao na vikao vya mazungumzo ya amani kama vile Camp David, Sharm al-Sheikh na Mkataba wa Amani wa Oslo, lakini hii leo wanapambana dhidi ya Wazayuni, wakiongozwa na vijana." 

Sayyid Raisi ameongeza kuwa, moyo huu wa muqawama umetokana na damu za Mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, na damu za Mashahidi waliokuwa wakilinda Haram Tukufu katika nchi za Syria na Iraq. 

 

Tags