Aug 08, 2022 11:49 UTC
  • Mamilioni ya Wairani katika maombolezo ya Imam Hussein AS ya Siku ya Ashura

Mamilioni ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo wameshiriki kwenye vikao vya maombolezo ya kukumbuka dhulma waliotendewa mashahidi wa Karbala katika Siku ya Ashura.

Wananchi wa matabaka tofauti ya Iran wakiwemo vijana na wazee, wanawake kwa wanaume wameshiriki kwenye maombolezo hayo ya kukumbuka siku aliyouliwa shahidi Imam Hussein AS pamoja na masahaba zake 72 katika jangwa la Karbala.

Waombolezaji kote Iran wakiwa wamevalia nguo nyeusi kama ishara ya maombolezo walikuwa wakibubujikwa na machozi kwa majonzi na huzuni kwa dhulma iliyofanywa na madhalimu dhidi ya kizazi bora cha wanadamu.

Wairani wanaoshiriki katika maombolezo ya Siku ya Ashura husikiliza hotuba na mashairi kuhusiaiana na masaibu yaliyomkumba Imam Hussein AS huko Karbala. Katika siku hii idadi kubwa ya wafadhili hujitolea kuwalisha mamilioni ya waumini ambapo chakula hicho ni maarufu kama Nazri.

Mjumuiko wa maombolezo ya Siku ya Ashura, Tehran

Katika tukio la Karbala lililojiri katika siku kama ya leo mnamo mwaka 61 Hijria, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani alisisitiza na kueleza bayana kwamba: "Kusudio langu ni kuufichua na kuufedhehesha utawala ulio dhidi ya Uislamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya na kukabiliana na dhulma na uonevu."

Mafunzo ya harakati ya Imam Hussein AS yamesambaa na kutanda katika historia na jiografia ya viumbe, wanadamu na ulimwengu mzima na hayawezi katu kuishia kwenye mipaka maalumu.

Tags